TFF yaruka kimanga kuliwa fedha za Kombe la FA

Muktasari:

Mashindano ya Kombe la FA yaanzia hatua ya awali ngazi ya wilaya, mkoa na baadaye taifa na bingwa wake ndiye anayeiwakilisha Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika

Dar es Salaam.Wakati kukiwa na tetesi za kuchelewa kuanza kwa mashindano ya Kombe la FA, kwa madai ya fedha zilizokuwa zitumike katika mashindano hayo kutumiwa na Shirikisho la Soka (TFF) kwa majukumu mengine, Shirikisho hilo limeluka kimanga tuhuma hizo huku likieleza hatma ya mashindano hayo.

Awali kulikuwa na taarifa za chini chini kuwa mashindano hayo yaliyokuwa yaanze Oktoba kwa hatua za awali yameshindwa kuanza kutokana na mkanganyiko wa fedha zinazotolewa na mdhamini wa mashindano hayo.

Taarifa zaidi zilidai TFF ilikopa fedha kutoka mfuko wa mashindano hayo hivyo kuna uwezekano mdhamini hana fedha nyingine ya kuwapa ndiyo sababu ya kuchelewa kuanza kwa mashindano.

Mkurugenzi wa mashindano wa TFF, Salum Madadi alipoulizwa kuhusu madai hayo na kinachoendelea kuelekea kwenye mashindano hayo alisema hakuna ukweli kwani kama fedha za FA zingekuwa zimekopwa wala wasingekaa kimya.

"Mashindano yameanza tayari katika ngazi za wilaya na tunatarajia kati ya Januari yawe yameanza kwenye ngazi ya taifa, hayo yanayozungumzwa hayana ukweli wowote," alisisistiza Madadi.

“Kama kuna fedha ambayo imekopwa kutoka mfuko wa mashindano hayo basi watatolea ufafanuzi, lakini hakuna kitu kama hicho sasa,” alisema Madadi.

Awali mmoja wa vigogo kutoka shirikisho hili aliuambia mtandao huu kuwa hali ni mbaya na yote yanayosemwa kuhusu mashindano hayo yana ukweli.

"Wacha twende hivyo hivyo, lakini jambo hili lilivyokaa hali ni mbaya," alisema kigogo huyo akiomba hifadhi ya jina kutokana na nafasi aliyo nayo katika usimamizi wa mashindano hayo.