Waliomlilia kocha Masoud Djuma, ghafla tu wamenyamaza zao

Muktasari:

Zinakuja hisia kwamba huenda makocha waliofukuzwa na Simba chini ya usaidizi wa Masoud walikuwa wazuri, lakini walikuwa wanahujumiwa na kocha huyu kijana

Dar es Salaam.MTU anayeitwa Masoud Juma, popote alipo, hafurahishwi na matokeo ya Simba. Wakati mashabiki wakifurahia, yeye amenuna. Wakati mwingine makocha au wachezaji sio wazalendo kuliko mashabiki. Amini katika ushabiki wa mashabiki, sio makocha na wachezaji.

Simba inashinda kadri inavyojisikia. Na bahati nzuri inashinda huku ikicheza vema kweli kweli. Inawalazimisha maadui kukaba kwa muda mwingi. Inatengeneza nafasi nyingi za kufunga. Mashabiki wanaondoka wakiwa wanacheka.

Kwa sasa ukitoka katika mechi za Simba hauwezi kujua ni nani alikuwa shabiki wa kocha msaidizi aliyepita, Masoud Juma na nani hakuwa nyuma yake. Huu ndio unafiki wetu katika ubora wake. tutachukua muda mrefu kuufahamu mpira.

Alichofanya Masoud Juma ilikuwa ni kuwageuza akili mashabiki wa Simba. Kuna mechi ambazo timu ilicheza vema chini yake wakati ikiwa katika kipindi cha mpito. Baada ya hapo akawateka akili mashabiki. Alipogundua kuwa kuna baadhi ya kundi la mashabiki lipo nyuma yake akatumia nafasi hiyo kukiuka weledi wa kazi ya ukocha.

Hakuna mtu ambaye alijikumbusha kwamba Masoud Juma aliachiwa timu katika michuano ya SportPesa Super Cup pale Kenya na timu haikufunga walau bao moja. Wote walisahau na kuanza kusifu zaidi ubora wa kocha Msaidizi.

Katika kazi ya ukocha, ukiwa kocha msaidizi jukumu lako kubwa ni kusapoti mawazo ya kocha mkuu. Ni kumsaidia kocha mkuu katika kile ambacho anataka. Masoud alionekana kutamani nafasi ya Ukocha mkuu na badala yake akaachana na weledi wa taaluma yake.

Waliomsaidia aachane kabisa na weledi wa taaluma yake ni mashabiki na wanachama wafuata upepo ambao kwa sasa wametoweka. Wao ndio walikuwa wanashinda mitandaoni kuivuruga timu yao. Leo wametoweka zao.

Kuna wakati niliandika makala ambayo niliwataka Simba wachukue maamuzi mazito. Ama kumfukuza Masoud Juma au wampe ukocha mkuu. Hakutaka tena kuwa kocha Msaidizi na Simba isingefanikiwa kama angeendelea kuwepo katika nafasi yake.

Kocha wa sasa wa Simba, Patrick Aussems alihitaji muda kukisuka kikosi chake. Wasifu wake wa kazi unajieleza wazi. Haiwezekani kocha akaichukua timu iliyobadili kikosi chake mara kwa mara halafu akaanza kwa kupata mafanikio.

Inachoonekana kwa sasa baada ya Simba kushinda mechi zake kwa idadi kubwa ya mabao ni kama vile wanaelewa kile ambacho kocha anataka. Ni wazi kwamba imani ya mashabiki kwake imeanza kujengeka kiasi kwamba hata kama Simba ikifungwa mechi moja sidhani kama atarushiwa mawe na chupa za maji kama ilivyotokea katika pambano dhidi ya Mbao FC pale Mwanza.

Kilichotokea Mwanza kilitokana na uchawi ambao Masoud Juma aliutengeneza dhidi ya mashabiki wa Simba waamini kwamba timu bila ya yeye haiendi. Lakini sasa wataelewa kwamba kocha yeyote ambaye anatua klabuni anahitaji muda kutimiza mipango yake.

Kuna makocha ambao wanajiwekea malengo ya muda mfupi katika kutimiza malengo yao na kuna makocha ambao wanajiwekea malengo ya muda mrefu katika kutimiza wanachokitaka. Haijalishi una wachezaji wenye ubora kiasi gani, mwisho wa siku unatengeneza timu ambayo itachezesha wachezaji 11 tu kwa ajili ya kushinda mechi.

Badala yake Masoud Juma alihakikisha kwamba Aussems hatimizi malengo yake na muda wote mashabiki wanamuwaza yeye zaidi badala ya kuwaza mipango ya kocha mkubwa. Ni kosa ambalo hauwezi kuliona katika klabu za wenzetu.

Zaidi ni kosa ambalo linaloendelea katika soka. Kwanini mpaka leo tuna makocha wasaidizi wa kudumu? Kwanini kocha mmoja Msaidizi anawatumikia makocha wakubwa watatu hadi wanne tofauti? Ndio maana wenzetu wanawawajibisha makocha kwa sababu wanawaachia uhuru wa kufanya kazi zao.

Ni kama ilivyo sasa kwamba ni rahisi kwa Simba kumuwajibisha Mzungu wao kwa sababu wamemuachia kila kitu katika timu. Lakini pia zinakuja hisia kwamba huenda makocha waliofukuzwa na Simba chini ya Usaidizi wa Masoud Juma walikuwa wazuri lakini walikuwa wanahujumiwa na kocha huyu kijana ambaye alikuwa anatamani kazi ya mabosi wake.

Ujumbe wangu wa leo ni kwamba mashabiki tuache kufuata upepo katika masuala la kitaalamu ambayo hatuyafahamu sana. lakini pia kwa mwenendo wa soka letu mpaka sasa nadhani kuna umuhimu kwa klabu kama ya Simba baada ya mabadiliko yao ya kiutawala huu huenda ukawa wakati sahihi kwao kuwa na mtu anayeitwa Mkurugenzi wa Ufundi.

Mtu mwenye weledi wake ambaye anaweza kuyatazama mambo kiufundi zaidi. Ni mtu ambaye angeweza kuchukua maamuzi kama haya ambayo viongozi wa Simba walichelewa kuyachukua kwa Masoud Juma na badala yake wakaacha mpaka athari zake zilipoonekana Mwanza wakati kocha mkuu alipopigwa chupa kwa sababu mashabiki wanaamini zaidi katika kocha msaidizi. Katika soka la kisasa hakuna kitu kama hiki.