Wema afungiwa miaka miwili kujihusisha na filamu

Monday October 29 2018

 

By Elizabeth Edward

Dar es Salaam. Chama cha waigizaji mkoa wa Kinondoni (TDFAA) kimemfungia mwanachama wake Wema Sepetu kujihusisha na masuala ya filamu kwa muda wa miaka miwili.

Huo ni mwendelezo wa adhabu kwa muigizaji huyo kufuatia kusambaa kwa video inayomuonyesha akifanya vitendo vinavyokinzana na maadili ya Mtanzania.

Chama hicho kimekwenda mbali zaidi na kutaka Mamlaka za kiserikali zipuuze utetezi unaotolewa na muigizaji huyo kwa kuwa una lengo la kuvipumbaza visimchukulie hatua.

Msemaji wa chama hicho Masoud Kaftany ameeleza kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kamati ya maadili kujadili suala hilo kwa kina.

“Hii si mara ya kwanza kwa Wema kufanya mambo ya ajabu, aliwahi kuanika video ya makalio tukamuita akaomba radhi, safari hii ndio amefanya haya.

Amesema kamati imeunga mkono hatua zilizochukuliwa na bodi ya filamu na imeliomba Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) kumuongezea adhabu itakayomzuia asijihusishe na shughuli zozote za sanaa kwa kipindi cha miaka miwili.

Katibu Msaidizi wa chama hicho Herrieth Chumila amesema baada ya picha hizo kuanza kuzagaa walifanya jitihada za kumtafuta msanii huyo lakini hazikuzaa matunda.

“Tulimuita akasema yupo Burundi ila tunafahamu haikuwa kweli kama kwamba haitoshi leo pia tulimuita aje hapa lakini hajatokea hadi muda huu,”

Chumila ameeleza kuwa kamati hiyo ipo macho kwa wasanii wake hivyo waache matendo yanayoweza kuchafua taswira ya sanaa na taifa kwa ujumla.

Advertisement