NO AGENDA: HILI LA MO! UKINUNA UWE NA SABABU

Mohammed Dewji

TUNASHAURIWA “ukinuna uwe na sababu”, sio unanuna tu hata watu hawajui kinachokufanya unune. Kununa bila sababu ni uchawi, maana unakuwa na sababu zako ambazo wengine hawazioni kwa macho ya kawaida.

Ulimpigia goti kigagu wako amtengeneze bosi wako, na pesa umetoa. Mara unakutana naye akiwa mwenye afya timamu. Hapo lazima unune, sababu ya kununa itakuwa siri yako. Usiku mzima umezisujudia tunguli ili bosi fulani asiamke. Unamshuhudia akiwa buheri! Utanuna na utasonya bila sababu iliyo wazi.

Ukinuna uwe na sababu; mfano unawahi ibada halafu foleni barabarani zinakuchelewesha, hapo ni haki kununa. Mwenye nyumba unayemsumbua kumlipa kodi, anakwambia uwahi akupe mkataba wa bure kama sadaka uishi mwaka mzima, halafu bosi wako anakuchelewesha ofisini mpaka mwenye nyumba anaghairi.

Hapo ukinuna unakuwa na sababu. Na ukiisema watu watakuelewa. Sio unabeti MO Dewji hatapatikana halafu amepatikana. Hapo ukinuna utajieleza nini? Sana sana ukiulizwa sababu ya mnuno wako utajibu “ aah! basi tu”. Maana imekaa kichawichawi.

Pengine baada ya kusikia familia ya MO Dewji imetangaza dau la Sh1 bilioni kama zawadi kwa ambaye angefanikisha kupatikana kwake au kwa yule angetoa taarifa ambazo zingewezesha kumpata, nawe uliingia chimbo. Ukalala kaburini na kuita mizimu, ukaibusu hirizi ya bibi yako ili ufunuliwe alipo ulambe bilioni. Mara unapokea taarifa kuwa watekaji wamemtupa MO Gymkhana, Dar. Hapo utanuna kukosa bilioni ila sababu hiyo si ya msingi.

La maana ni kwamba MO kapatikana. Ni furaha kwa Watanzania kuona ndugu yao amerejea kutoka mikononi mwa wahuni fulani. Jumuiya ya wapenda soka inakenua tu, maana MO ni mdau mkubwa wa soka. Mashabiki wa Simba huwaambii kitu sasa, kwani Underground King wao amesalimika.

Hivyo basi, baada ya siku tisa zenye maumivu makubwa ya kutojua mahali alipo, hatimaye furaha. Nchi ipo shereheni. Ni sherehe ya kushindwa kwa watekaji na kushinda kwa Tanzania. Sasa tukikuona umenuna bila sababu ya msingi, na tukikuuliza unajibu “basi tu”, tutakachofanya ni kukuunganisha na waliomteka MOo. Hao ndiyo kwa sasa wananuna!

Iwe ulibeti kuwa MO hatapatikana au unaumia kuikosa bilioni, ukinuna unakuwa sawa na watekaji. Wao ndiyo wananuna. Na siku zote wamekuwa wakivinunia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, kwamba wana kiherehere. Walitaka suala la kumteka MO liende kimyakimya.

NAOMBA KUSEMA NA MO

Karibu MO kwenye uhuru wako uliouzoea. Umemshukuru Mungu na umewashukuru Watanzania wenzako. Pengine umeambiwa kuhusu mshikamano wa Watanzania katika suala lako. Hapa ndipo ninapotaka kusema na wewe.

Ni kweli Watanzania walishitushwa na tukio la kutekwa kwako. Waliumia mno. Walikuombea na hawakushusha sauti zao katika kudai ili vyombo vya ulinzi na usalama viwajibike ipasavyo mpaka upatikane. Wapo wanaoishi Tanzania na wengine nje ya nchi. Wengi, isipokuwa wachache, walipaza sauti kutaka urejeshwe.

Mshikamano wa Watanzania wengi, kasoro wachache walioleta utani, ni kipimo cha upendo mkubwa walionao kwako. Zaidi, Watanzania ni watu wazuri, wanapenda amani. Hawapendi kuona nchi yao inachafuliwa. Hawapo tayari kumwona mwenzao akidhuriwa kwa sababu yoyote ile.

Si pesa zako zilizowafanya Watanzania waungane kudai urejeshwe. Watanzania asili yao hawazuzuliwi na pesa. Wao hujali utu kwanza. Waliungana kwa ajili yako kutokana na ukweli kwamba umekuwa mtu mzuri kwao. Hujikwezi kisa wewe ni tajiri. Unajichanganya na watu wa kawaida na unazungumza nao lugha moja.

Ukiwa mwekezaji ukimiliki hisa asilimia 49 za Klabu ya Simba, umekuwa ukijipambanua kuwa shabiki wa klabu hiyo kuliko bosi. Jumuiya ya mashabiki wa Simba hukuona wewe ni mwenzao. Hili lina mguso mkubwa zaidi ndani ya nyoyo zao.

Umekuwa shabiki na mhamasishaji wa Taifa Stars. Umefanya mengi kwa kuidhamini timu ya taifa na kuishabikia kwa ‘ukichaa’ kuliko mabilionea wengine. Naweza kuthubutu kuwa hakuna kiongozi wa serikali na hata wa soka nchini, ambaye amewahi kufanya japo nusu yako.

Kupanda juu ya gari la wazi pamoja na wachezaji wa Taifa Stars, ukiwa kifua wazi, kuonyesha furaha yako kwa ushindi, ni kielelezo kwamba unaipenda sana Taifa Stars. Unaipenda mno nchi yako. Wewe ni mzalendo wa kweli. Na kwa ‘ukichaa’ ule, jumuiya ya wapenda soka nchini hukuona wewe ni mwenzao.

Ndiyo maana walipaza sauti kwa nguvu kudai urejeshwe. Walionywa wasiseme lakini hawakukaa kimya. Wangenyamaza vipi wakati hawakuwa wakijua mahali ambako mwenzao ulipokuwa? Wewe ni mwenzao. Wanakupenda sana kama unavyowapenda.

Nakuhakikishia MO; kama unadhani Watanzania walipaza sauti kwa sababu wewe ni tajiri, atokee atekwe tajiri mwingine ambaye hajabeba mapenzi ya Watanzania kisha uone. Hata ikitokea zikawepo sauti za kudai arejeshwe, hazitabeba uzito sawa na zilizopazwa kwa ajili yako.

WATANZANIA WAMESHINDA

MO ameshinda sana. Hata hivyo, Watanzania wameshinda zaidi kwa watekaji kumwachia MO. Sifa ya nchi inaharibiwa na matukio ya kihuni. Kutekwa tu ni sifa mbaya, ila kupatikana kwake kunarejesha heshima.

Watanzania wameshinda kwa sababu wameonesha mshikamano. Wamewaonesha watekaji kwamba kila Mtanzania ni Mtanzania. Ukimgusa yeyote wataamka kumdai. Ushindi huu ni mkubwa sana mbele ya watekaji na katika uso wa dunia.

Kuna mfululizo wa matukio ya watu kupotea. Kada wa Chadema, Ben Saanane anakaribia miaka miwili tangu atoweke. Mwandishi wa habari, Azory Gwanda ana miezi 11 sasa tangu alipotoweka. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Kigoma, Simon Kanguye hajulikani alipo.

Mwana Hip Hop, Roma Mkatoliki na wenzake watatu walitekwa mwaka jana wakaachiwa baada ya kelele nyingi. Ukifuatilia mnyororo wa utekaji unabaini kwamba watekaji hawaangalii yeyote, awe tajiri au maskini, mwanasiasa na asiye mwanasiasa. Wanateka tu!

Hisia za karibu zaidi kwa Watanzania walio wengi ni kwamba Saanane, Azory na Kanguye nao walitekwa. Kama hivyo ndivyo ilivyo, maana yake kama MO angeondoka jumla, ingethibitika kuwa wateka watu Tanzania wana nguvu kiasi kwamba, wanaweza kumchukua yeyote na kumpoteza. Hili hawajafanikiwa.

Rejea namna nchi ilivyokuwa alipotekwa Roma na wenzake watatu. Bunge lilivyoamka, wasanii walivyoungana na mitandaoni kulivyochafuka. Kisha Roma na wenzake waliachiwa. Ona mshikamano ulivyoonekana alipotekwa MO. Kisha MO ameachiwa.

Jawabu ni kwamba kumbe Watanzania wakiungana kupaza sauti, huwaogopesha watekaji. Basi mshikamano wa aina hii uendelee wakati mwingine wowote. Akipotea Mtanzania, imguse kila Mtanzania. Kugawanyika hutoa nafasi kwa wahalifu kusimika mizizi ya uhalifu wao.