TUTUMIE MCHORO WA PENTAGONI KUMSAKA MO DEWJI NA WATEKAJI

Mtanzania anayeaminika kuwa tajiri namba moja nchini, Mohammed Dewji

Muktasari:

Kitendo cha Mo kutekwa kinaleta maswali mengi kuhusu Tanzania mpya. Ni kwa sababu kuna matukio kadhaa ambayo yametokea kuanzia mwaka juzi. Novemba 2016, kijana wa Kitanzania, Ben Saanane alitoweka na mpaka leo hajulikani alipo na hatama yake ni nini. Novemba mwaka jana, mwandishi wa Mwananchi, Azory Gwanda alitoweka.

THE Pentagon ni makao makuu ya idara ya ulinzi Marekani, yaliyopo Arlington County, Virginia. Pentagon ni umbo lenye pembe tano. Majengo ya makao hayo makuu ya ulinzi Marekani, yamejengwa kwa ramani ya pembe tano, ndiyo maana yanaitwa Pentagon.

Inawezekana nimeanzia mbali. Twende hivi; pentagon ni umbo la pembe tano. Tuliandike Kiswahili; pentagoni. Sasa basi, Mtanzania anayeaminika kuwa tajiri namba moja nchini, Mohammed Dewji, alitekwa Oktoba 11, mwaka huu. Ilikuwa saa 11 asubuhi. Hoteli ya Colosseum, Oysterbay, Dar es Salaam.

Kwa nini Colosseum? Jibu ni kwamba alikwenda mazoezini. Ni kawaida yake kutumia gym ya Colosseum kufanya mazoezi. Ni sawa na kusema kuwa ni rahisi kumtega Mo Colosseum na kumpata. Hii inaondoa shaka ya kwamba labda alivutwa eneo husika ili watekaji wapate unafuu wa kumteka. Tungejiuliza; aliyemtega ni nani?

Tuchore pentagoni yetu na tumuweke Mo katikati kisha tuanze kuchekecha nadharia. Pentagoni inawezesha kumchambua Mo, yeye ni nani, kwa nini atekwe, mazingira ya usalama wa nchi, tulipotoka, tulipo na uchambuzi wa akina nani ni watekaji. Kila pembe ina mantiki. Pembe ni tano.

PEMBE YA KWANZA

Mo ni nani? Jibu; ni mfanyabiashara tajiri. Historia ya utajiri wake haina utata kusema labda anaweza kuwa kuna watu aliwazidi ujanja nyakati za utafutaji, kwa hiyo wanamteka ili kumlazimisha awape chao au kulipa kisasi. Mo ni mtoto wa kishua mwenye akili. Alikuta mali nyumbani na kuziendeleza.

Baba yake, Gulamabbas Dewji ni bilionea na ndiye mwanzilishi wa kampuni za Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL). Jarida la Forbes Afrika liliandika mwaka 2013 kuwa Mo alikuta mtaji wa kama Sh50 bilioni mwaka 1998 kisha yeye akapiga kazi kisomi na kwa maarifa mengi hadi kufikia zaidi ya Sh3 trilioni ndani ya miaka 15.

Mo ni wa kishua kweli. Alisoma Shule ya Msingi Arusha, sekondari akasoma Tanganyika International School. Mwaka 1992, Mo alipokuwa na umri wa miaka 17, baba yake alimpeleka kusoma Marekani. Alianzia shule ya mchezo wa golfu ya Arnold Palmer, Florida kisha akasoma High School shule mbili za Florida, Trinity Preparatory na Saddle Brooke.

Alisoma Chuo Kikuu cha Georgetown, Washington DC, alikotunukiwa ganda lake la biashara za kimataifa na fedha. Mo pia amesoma dini. Hapa sasa unaweza kujiongeza kujua ni kwa nini Mo ni tajiri lakini mnyenyekevu. Aliwahi kusema alipomaliza chuo alijaribu kufanya kazi Marekani, kabla kuamua kurejea nchini ili kutumikia kampuni za familia yake.

Ni mwanamichezo hasa. Ni shabiki lialia wa Simba. Hivi sasa ni mwekezaji wa klabu hiyo akimiliki hisa asilimia 49. Amekuwa msaada na mdhamini wa Simba na Taifa Stars. Juni 16, 2007, Taifa Stars iliipiga Burkina Faso nyumbani kwao bao 1-0, lililozamishwa na Erasto Nyoni. Mchezo ulikuwa wa kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2008.

Baada ya ushindi huo, Mo wakati huo akiwa mlezi wa Taifa Stars na mdhamini vilevile, aliungana na wachezaji kwenye gari la wazi, akawa kifua wazi pamoja na wachezaji, gari likasindikizwa na umati kwa maandamano. Hapa unajionea kuwa Mo ni tajiri msela, mtu wa kujichanganya. Zaidi, Mo aliwahi kuwa mmiliki wa Klabu ya African Lyon lakini akaitosa.

Mo ni mhisani. Ana mfuko wake wa kusaidia ustawi wa maisha ya Watanzania unaoitwa Mo Dewji Foundation. Katika tovuti ya mfuko huo, anasema yeye amebarikiwa fedha, hivyo lazima atoe. Nukuu yake ni hii: "Mungu anapokubariki kifedha, usinyanyue kiwango chako cha kuishi, nyanyua kiwango chako cha kutoa." Hapa unaona Mo si mbinafsi.

Si mbaguzi. Ungemuona gym akipiga picha na watu mbalimbali wa kawaida. Tabasamu lake lipo karibu. Mchangamfu. Mo ni mtu ambaye kila mmoja angependa awe rafiki yake. Wanaohoji kwa nini hatembei na ulinzi mkubwa, alishawapa jibu kabla hajatekwa, kwamba; ukibarikiwa fedha usijikweze, saidia wengine.

PEMBE YA PILI

Tuitazame Tanzania ilipotoka na ilipo. Miaka michache nyuma, Tanzania iliwahi kukumbwa na magomvi ya wafanyabiashara. Reginald Mengi alitifuana na baadhi ya wenye asili ya Asia. Mengi aliwataja Rostam Aziz, Tanil Somaiya, Yussuf Manji, Jeetu Patel na Subhash Patel kuwa ni mafisadi papa.

Kitendo hicho cha Mengi kilisababisha mahakama ziwe na hekaheka, wafanyabiashara hao kushtakiana. Hakuna tukio la kutekana wala kupigana risasi lililotokea. Unaona kuwa Tanzania ilikuwa nchi ya watu ambao wakikorofishana, kimbilio lao ni mahakamani. Hakukuwa na kutekana.


Aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibondo, Simon Kanguye, alitoweka tangu mwaka jana. Mwanamuziki wa Hip Hop, Roma Mkatoliki, alitekwa na wenzake watatu mwaka jana, wakaachiwa baada ya siku tatu. Je, Mo naye ni wa mkondo huo? Atarudi?

PEMBE YA TATU

Mo hajawahi kudhihirika kuwa na mgongano wa kibiashara na wafanyabiashara wenzake. Daima huonekana mtu asiye na makuu. Na inaonekana mwenyewe hujiamini hana maadui ndiyo maana huwa habebani na walinzi, japo uwezk wa kujaza walinzi hata mamia anao.

Kwa historia yake ya kimaisha, anavyoishi kawaida na hata wakati mwingine kupanda bodaboda au kutembea kwa miguu bila ulinzi, kuna maswali yatakuja kichwani. Nani adui asiyetambulika anaweza kuwa nyuma ya kutekwa kwake?

Lakini swali kubwa ni je, hii Tanzania imekuwaje? Katoweka kada wa Chadema (Saanane), kapotea wa CCM (Kanguye), hajulikani alipo mwandishi wa habari (Azory), walitekwa Roma na wenzake, sasa ni Mo. Vyama tofauti, kazi hazifanani. Wanamuziki, wanasiasa, mwandishi, mfanyabiashara. Kama ni utekaji mbona hakuna kundi mahsusi linalolengwa?

PEMBE YA NNE

Tuguse nadharia ya kisiasa. Mo aliwahi kuwa mbunge wa Singida Mjini miaka 10, na aliacha mwenyewe, maana hakugombea mwaka 2015. Hata hivyo, Mo pamoja na kuacha siasa bado ni kada wa CCM, lakini pia ni rafiki wa wanasiasa mbalimbali.

Ukiwaza vizuri, utapata nadharia hii; je, kuna mtu ambaye anaweka mikakati ya uongozi siku zijazo na Mo ndiye anamuwezesha? Ukiliwaza hilo hutaacha pia kumfikiria anayemwona Mo ni tishio. Siasa zina mambo mengi sana. Vema kuwaangaza wanasiasa marafiki wa Mo na maadui zao.

Utekaji ni moja ya vitendo vya ugaidi. Je, kuna watu wanataka kuitetemesha Serikali, kwa hiyo wameona wamteke mfanyabiashara mwenye mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa? Ukiwaza hivyo, utajiuliza baada ya Mo nini wanataka kifuate?

PEMBE YA TANO

Tutazame nadharia za kibiashara. Tumeshaona kuwa Mo haonekani kuwa na maadui. Siku zote yupo mbali na migogoro. Hata hivyo, haya maisha unaweza kuwa unajiona huna adui kumbe wapo tele na wamekuzunguka. Je, ni uwekezaji wake Simba ndiyo tatizo?

Kuna watu anadaiana nao? Hivi karibuni aliandika kwenye akaunti yake ya Twitter kuwa mikopo huvunja urafiki. Hiyo 'twiti' inahusika na kutekwa kwake? Je, kuna watu wa karibu aliwakopesha fedha na wanamsumbua kurejesha?

Tuorodheshe biashara zake. Bidhaa za viwanda vyake. Masoko yake ni yapi? Washindani wake wa kibiashara ni akina nani? Dunia imejaa visa vingi, unaweza kuchekeana na mfanyabiashara mwenzako ukadhani amani imetawala, kumbe chuki imejaa moyoni.

Hapohapo kwenye biashara; je, kuna wafanyakazi walioachishwa kazi kwenye kampuni zake? Mtaalamu wa mifumo ya kibenki Marekani, John Grundhofer, alitekwa mwaka 1990. Nadharia mojawapo ikawa ni wafanyakazi wengi walioachishwa kazi kwa sababu ya mfumo aliouanzisha alipojiunga First Bank System.

Mwisho ni fedha. Mo ni tajiri anayewika Afrika. Na hajaufanya mtindo wa maisha yake kuwa tata. Je, watu wameona kwa vile hana ulinzi wamemteke ili kujipatia pesa kihuni? Tusiache kujiuliza kuhusu mapenzi. Ya Mungu ni mengi. Muhimu ni kumwombea, waliomteka wanaswe na Mo mwenyewe arejee salama.