Kashfa ya dawa za kusisimua misuli janga Kenya

Friday October 12 2018

 

Nairobi, Kenya. Kashfa ya matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku michezoni zikiwemo za kusisimua misuli imezidi kuathiri mchezo huo nchini Kenya.

Hiyo inatokana na kufungiwa miaka minne kujihusisha na riadha kwa mwanariadha chipukizi wa mbio ndefu za marathon, Samuel Kalalei baada ya kufeli vipimo vya damu.

Mwanariadha huyo mwenye miaka 23, alifeli vipimo alivyofanyiwa Aprili mwaka huu katika mbio za Rotterdam Marathon nchini Uholanzi.

Kalalei, alikuwa akijiandaa kujiwekea muda bora zaidi katika mbio ndefu baada ya mwaka jana kutwaa ubingwa wa Athens Marathon.

Kalalei alisimamishwa Juni mwaka huu kujihusisha na riadha akisubiri uamuzi wa matokeo ya uchunguzi wa vipimo na baada ya majibu kutoka na kubainika kuna chembe chembe za dawa zilizopigwa marufuku amefungiwa.

Huyo anakuiwa mwanariadha wa tatu wa Kenya kufungiwa tangu Novemba mwaka 2017 wa kwanza alikuwa Asbel Kiprop, aliyefungiwa Novemba 2017.

Pia, bingwa wa zamani wa Olimpiki katika mita 1500 na mshindi mara tatu wa Dunia, Jemima Sumgong wamefungiwa kwa miaka minne.

Septemba mwaka huu wakala wa kupambana na matumzi ya dawa zilizopigwa marufuku michezoni duniani (Wada), alisema kuwa kuna tatizo kubwa mno la matumizi ya dawa hizo nchini Kenya.

Advertisement