Dereva Uber asimulia kutekwa Mo Dewji

Thursday October 11 2018

 

By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Dereva wa Uber amesimulia tukio la kutekwa kwa mtu mmoja jijini Dar es Salaam ambaye amedai kuwa alimtambua kuwa ni mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji.

 Dereva huyo, ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema alikuwa akienda kumshusha abiria katika Hoteli ya Collesssium saa 11 asubuhi ndipo alipokutana na tukio hilo.

 “Tulikuwa tunakaribia eneo hilo, mara mbele yetu tukaona watu  wanne wameshuka kwenye gari dogo wakiwa wamejifunika usoni, wakapiga risasi moja juu, wale askari wa hoteli kila mmoja akakimbia,” anasimulia.

 “Waliingia ndani ya hoteli na kutoka na mtu, ambaye nilimjua kuwa ni Mo,” anasimulia dereva huyo ambaye anadai muda mwingi alikuwa amejiinamia kwenye gari akihofia.

 Inadaiwa waliingia sehemu ya kufanyia mazoezi ‘gym’ na kumkuta hapo huku wakiwaacha watu wengine waliokuwa hapo.

 Anasema baada ya watu hao kumchukua mwekezaji huyo wa klabu ya Simba waliondoka na gari kwa kasi kuelekea maeneo ya Masaki.

 Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema polisi wanafuatilia taarifa za madai ya kutekwa kwa mfanyabiashara huyo.

 Akizungumza na MCL Digital leo Alhamisi  asubuhi Mambosasa amesema baada ya kupata taarifa za tukio hilo wanafuatilia kujua ukweli wake.

Dewji ni mwekezaji wa klabu ya Simba akiwa na hisa 49 na amekuwa akiingia katika chati ya juu ya jarida la Forbes kama miongoni mwa matajiri vijana Afrika.

 

Endelea kufuatilia MCL Digital kwa taarifa zaidi

 

Advertisement