Kerr: Ratiba hii inachosha, KPL legezeni kidogo

Wednesday August 15 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi, Kenya. Wakiwa wameshaingia dimbani mara tano katika mwezi huu wa Agosti pekee, hatimaye Kocha mkuu wa mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Kenya, Muingereza Dylan Kerr amefunguka na kuitaka bodi ya  KPL, kuangalia upya ratiba za mechi, kwa kile alichosema kuwa inachosha.
Kauli ya Kerr imekuja wakati ambapo kwa mujibu wa msimamo ulivyo hivi sasa, mabingwa hao mara 16 wa KPL, ambao wanaongoza msimamo wakiwa na pointi 60 kileleni, mechi tatu mkononi huku wakiwazidi wapinzani wao wa Karibu Bandari FC kwa jumla ya pointi 12.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuishushia kipigo cha mbwa mwizi klabu ya Kakamega Homeboyz, katika mechi kali iliyopigwa Agosti 13 huko mjini Kisumu na kumalizika kwa ushindi 3-1, Kerr alisema nyota wake wanaonesha kuchoka hasa kutokana na kutokuwa na muda mzuri wa kupumzika.
''Tumechoka, tuna ratiba ngumu sana na inayochosha kwa kweli, kucheza mechi kila baada ya siku tatu sio kazi rahisi, inahitaji punzi. Mwezi huu tu tumeingia dimbani mara tano, huu ni mzigo mkubwa kwa vijana. Ubaya zaidi tunahitajika kusafiri sana, naiomba KPL iangalie upya hili swala," alisema Kerr na kuongeza.
"Tuna mechi za nyumbani, tatu ni kiporo, bado pia tunahitaji kusafiri. Alhamisi tunakipiga na Chemelil wakati huo huo tunatakiwa kujiandaa kwa ajili ya Rayon, hii sio haki hata kidogo, vijana wanahitaji kupumzika sasa, ukiangalia namna tulivyocheza utashangaa sana na kwa hilo pia nawapongeza sana."
Ni katika kipindi hiki cha mrundikano wa mechi ambapo Kogalo walijikuta wakitobolewa kwa mara ya kwanza msimu huu baada ya kuchapwa 2-1 na Bandari FC, lakini pia ratiba inaonesha kuwa waba kibarua cha kuwakabili Rayon Sports katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika na baadaye kuwavaa Sofapaka na AFC Leopards, kwenye ligi.

Advertisement