Fatma Mustafa : 'Kitu nini' nyota Ligi Kuu wanawake, apania kuivunja rekodi yake msimu ujao

Thursday August 1 2019

 

By Olipa Assa

FATUMA Mustapha ‘Kitu nini’ alimaliza msimu uliopita akiwa na bao 39 kwenye Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara na timu yake ya JKT Queens iliibuka na ubingwa bila ya kupoteza mchezo hata mmoja, ameanza kujifua na msimu mpya akiweka wazi kutaka kuvunja rekodi hiyo na kuandika mpya.

Fatuma ni kati ya wachezaji chipukizi kwenye soka la wanawake Tanzaia Bara, amesema anatamani kufanya vitu vipya kila msimu anavyoaminni vitafanikisha ndoto yake kufika mbali hasa kucheza nje ya mipaka ya Tanzania.

Anasema licha ya changamoto nyingi zilizopo kwenye soka la wanawake, hazimkatishi tamaa kuwa mfano wa kuigwa kwa miaka inayokuja, kuandika rekodi ya uwepo wake kwenye mchezo huo alifanya vitu vikubwa kama ilivyo kwa wanasoka wanaume, akimtaja Edibily Lunyamila, Zamoyoni Mogella na wengine wengi ambao wana heshima kwenye mchezo huo nchini.

“Unajua ninaowataja ni umri wa baba zangu, lakini tunawasoma mambo makubwa ambayo walifanya, najiuliza kwa nini majina yao yanaishi mpaka leo, nimebaini wamefanya vitu vikubwa ambavyo hata mimi natamani kuvifannya pia.

“Nilipoamua kuchagua soka kuwa kazi itakayokuwa inaniingizia ama kujenga uchumi wangu, niliangalia na changamoto ambazo zipo, sikutaka kuzikimbia badala yake nitamani ziwe njia ya watakaokuja nyuma yetu waweze kuwa na mafanikio makubwa kama ilivyo kwenye soka la wanaume.

“Msimu ulioisha nilitamani nichukue kiatu cha dhahabu lakini sikuweza kufikia malengo, kilienda kwa dada yangu Asha Mwalala ambaye alimaliza akiwa na bao 40 sio mbaya kwa kuwa nipo naye kwenye timu, pia hainizuii kuivunja rekodi yake nadhani hata yeye atafurahi kuona hilo.

Advertisement

“Hilo limekuwa funzo kwangu kuongeza juhudi ya mazoezi ambayo yataniweka fiti kutimiza ndoto ya kuvunja rekodi ya bao 39 nilizofunga, najua sio lele mama ila ndio itakuwa kipimo cha kazi zangu kuwa zina hatua gani kila msimu,” anasema.

Mbali na hilo, ameyaomba makampuni binafsi kujitokeza na kuwekeza kwenye soka la wanawake kwa madai hawatapata hasara kama wanavyodhani kutokana na jamii kwa sasa kuwaunga mkono.

“Zamani ilikuwa inaonekana soka la wanawake kama ni uhuni, waliotutangulia walitutengenezea njia ya kuishawishi jamii kwa sasa inaona kama kazi kama zilivyo nyingine, ndio maana tunapata mashabiki hata uwanjani kuja kutuunga mkono.

“Tumeamua kufanya kazi ili tusijiunge na makundi mabaya mtaani basi tuungwe mkono kama ilivyo kwa soka la wanaume, ili na sisi tuweze kuwa vizuri kiuchumi,” anasema.

Advertisement