Zahera amzidi akili Aussems

Friday December 7 2018

 

By CHARLES ABEL, THOBIAS SEBASTIAN NA CHARITY JAMES

MPAKA sasa si mashabiki wa Simba wala Yanga wanafahamu nini kinaendelea ndani ya kikosi cha kambi ya Jangwani.

Kasi ya Yanga msimu huu imekuwa tishio licha ya kubezwa kuwa na kikosi cha kawaida kutokana na kushindwa kufanya vurugu kwenye usajili kisa kikiwa kukabiliwa na ukata.

Lakini, tangu kuanza kwa Ligi Kuu Bara msimu huu, Yanga imekuwa ikishinda nje ndani katika mechi zake na mpaka sasa haijapoteza mchezo tofauti na wapinzani wao Simba, ambao wako nyuma kwa tofauti ya pointi 11 huku ikiwa na mechi mbili za kiporo mkononi.

Yanga inashuka dimbani mwishoni mwa wiki hii kuikabilia Biashara United kutoka Mara ikisaka ushindi ambao, utawafanya waendelee kukaa kileleni wakiwa na pointi 41.

Ushindi huo sio tu utawafanya waendelee kutamba kileleni mwa msimamo wa ligi bali pia utaendeleza rekodi ya kutopoteza mechi.

Yanga imeshinda mechi 12 na kwenda sare michezo miwili, rekodi ambayo imekuwa kero kubwa kwa Simba ambao wenyewe hadi sasa wameshapoteza mchezo mmoja na kwenda sare mara tatu.

Hata hivyo, kama Yanga ikishinda dhidi ya Biashara United huenda ushindi huo ukamweka kwenye wakati mgumu zaidi kocha wa Simba, Patrick Aussems na kikosi chake kwani, utatanua pengo la pointi baina ya timu hizo hasa kipindi hiki muhimu cha vita ya kuwania ubingwa.

Ushindi wa Yanga kwa Biashara United, utaifanya timu hiyo inayonolewa na Mwinyi Zahera kufikisha pointi 41 ambazo zitakuwa 14 zaidi ya zile za Simba.

Ingawa Simba itakuwa na mechi tatu mkononi, presha huenda ikawa kubwa kwa Aussems na jeshi lake kwani, watalazimika kupambana vita mbili ili kuweza kutetea ubingwa wao msimu huu huku Ligi ikizidi kuchanja mbuga.

Vita ya kwanza ambayo Simba watalazimika kuhakikisha wanaishinda ni ile ya kuziba pengo hilo la pointi ili wawe sawa na Yanga, ambayo kasi yake msimu huu imeonekana kutoshikika ikishinda nyumbani na ugenini.

Lakini, hata ikifanikiwa kuwafikia Yanga, Simba itakuwa na kibarua kingine cha kuhakikisha wanawapita watani wao wa jadi na kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hadi pale msimu utakapomalizika ili watetee taji lao.

Ni wazi kwamba hesabu za Simba ni kutaka kuona angalau hadi wanamaliza mzunguko wa kwanza, wamepunguza pengo la pointi, wapo sawa au wameizidi Yanga.

Hata hivyo, hesabu hizo sio nyepesi kwani aina ya mechi ambazo Yanga imebakiza kabla ya mzunguko wa kwanza, hazionekani kama zinaweza kumtibulia hesabu zake ukiondoa ile ya Azam FC pekee.

Ukiondoa mechi ijayo dhidi ya Biashara United na ile ya mwisho kwenye mzunguko wa kwanza dhidi ya Azam FC, Yanga itacheza pia na Mbeya City na Ruvu Shooting ambazo zimekuwa hazina rekodi nzuri ya kuibuka na ushindi mbele yao.

Zahera akoleza moto

Wakati Yanga ikiiweka Simba kwenye wakati mgumu, Zahera amesema anachokiangalia kwa sasa ni kuendeleza ushindi kwa kila adui anayekutana naye hadi anamaliza ligi na kuwapa Yanga taji la Ligi Kuu Bara. Pia, amesema mchakato wa usajili mastaa wa maana ndani ya kikosi chake utaendelea kuwa chini ya kamati husika na kazi yake itakuwa ni kupendekeza.

Akizungumza na Mwanaspoti, Zahera amesema tayari amekabidhi ripoti yake kwa uongozi ikiwa ni hatua ya kuendelea kukisuka upya kikosi chake wakati huu wa dirisha dogo la usajili.

Kuhusu usajili wa dirisha dogo Zahera alisema: “Nafahamu muda wa dirisha la usajili unaelekea mwisho, lakini sitaki kulizungumzia hilo kwa sababu lina kamati yake, hapa nazungumzia mipango ya timu.”

Umeme wa Ngassa

“Ngassa ni mchezaji mzuri na ni mpambanaji na natambua umuhimu wake kikosini kwetu, lakini siamini kama kukosekana kwake tunaweza kuyumba kwa sababu kuna wachezaji wanaweza kuziba nafasi yake,” alisema.

Zahera alisema katika mchezo wa Jumapili na Biashara atamrudisha Deus Kaseke.

Aussems ANAWAZA KIMATAIFA TU

Kocha wa Simba, Aussems alisema akili yake kwanza ni katika mashindano ya Kimataifa kwani mechi inayofaata watacheza dhidi ya Nkana Rangers wakiwa ugenini na wanatakiwa kufanya maandalizi ya kutosha.

“Nafahamu tupo nyuma ya pointi 11 dhidi ya wanaongoza ligi lakini kwa sasa siwezi kusema lolote kutokana tunacheza mechi za Ligi ya mabingwa Afrika kwa hiyo nikichanganya mambo mawili kwa wakati mmoja si sahihi haswa kwa wakati kama huu,” alisema.

Advertisement