Yusuph Macho: Upweke ulinikimbiza umangani-5

KATIKA sehemu nne za kwanza za makala haya na kiungo wa zamani wa Yanga, Simba, Mtibwa Sugar na Taifa Stars, Yusuph Macho ‘Musso’ tuliangazia nyota huyo alivyogeuka mganga wa kienyeji baada ya kustaafu soka na historia yake alivyokinukisha Jomo Cosmos, Afrika Kusini na alivyokwama Ubelgiji baada ya kukosa visa ya kuingilia England. Tuungane tena leo.

SAFARI YA UARABUNI

“Baada ya hapo nilikwenda Uarabuni, Oman na kujiunga na klabu za Mascut Club mwaka mmoja, AL Nahdha (Oruba) nikacheza misimu miwili, na kisha kusajiliwa na Oman Club ambako pia nilicheza misimu miwili.

“Nimekaa Oman nikicheza mpira kama miaka mitano. Maisha ya Oman yalikuwa mazuri, nimeishi kama nipo nyumbani na kupata mahitaji yote na baada ya hapo, niliamua kurudi nyumbani Tanzania ili kuendelea na mambo mengine,” anasema Macho.

UPWEKE UARABUNI

Anasema, sababu ya kuamua kurudi nyumbani ni upweke uliopitiliza akiwa kule.

“Asikwambie mtu, maisha ya nyumbani Tanzania ni mazuri watu huwa hawajui tu. Kuishi kwenye mataifa mengine ni shida. Kule unakuwa ni wewe peke yako kwa kila jambo. Lakini hapa unaweza kutoka sehemu kwenda kwa jamaa kuna kampani kwa ujumla,” anasema Macho.

AIPA UBINGWA KAGERA

Anasema, alitoka Oman na kurudi nchini kwa ajili ya mapumziko mwaka 2006, akajiunga na Kagera Sugar akaichezea kwa miezi mitatu.

“Kagera waliniomba kwa ajili ya mashindano yale ya Tusker 2006, tulikuwa na marehemu Omary Chang’a na kina Shamte Ally, kipa yule kutoka Uganda, Ben Kalama na yule straika Michael Katende chini ya kocha marehemu Sylivester Marsh,” alisema Macho.

“Kwangu ni kumbukumbu kwa sababu katika mashindano yale tulifanikiwa kuchukua ubingwa ambao ndiyo wa kwanza kwa Kagera na wa mwisho katika mashindano hayo makubwa.”

ASTAAFU soka AWA KOCHA

“Baada ya Kagera nilirudi tena Oman, lakini mara hii sikukaa kabisa kule, nikarudi Tanzania rasmi na kustaafu soka.

“Niliamua kuanza kusoma kozi za ukocha kwa sababu ndiyo zilikuwa ndoto zangu tangu nacheza mpira miaka ya nyuma. Nimesoma kozi ya awali Magomeni tulikuwa na kina Selemani Matola (kocha wa sasa wa Lipuli FC) ya pili 2013 tulisoma Benjamini Mkapa tulifundishwa na mkufunzi Meja Mingange na 2014 nilisoma Leseni C,” anasema Macho.

ANAFUNDISHA VIJANA

Anasema, pamoja na kufanya shughuli tofauti, asilimia 60 ya maisha anayoishi anapenda ukocha.

“Yaani, hivi ninavyofanya shughuli lakini jioni lazima niende kufundisha soka, ukiona nimepumzika labda naumwa. Kwa sasa huwa nawafundisha vijana wadogo pale Azam FC na Mbande FC,” anasema Macho.

“Nilikuwa nafanya hivyo kwa sababu nilitaka kupumzika kwanza lakini kwa sasa nataka nianze rasmi kufundisha timu za wakubwa kwa sababu malengo yangu ni kuwa kocha mkubwa, malengo ambayo niliyaweka wakati naanza kucheza.”

ATAKA UKOCHA STARS

Anasema, mbali na shughuli anazofanya, ndoto zake ni kuwa Kocha wa Taifa Stars na si ilimradi kocha bali mwenye mafanikio makubwa kama au zaidi ya aliyopata Emmanuel Amunike aliyeipeleka Tanzania kucheza AFCON 2019 nchini Misri.

“Kama nilivyodhamiria kuwa mchezaji mkubwa hapo nyuma ndivyo nilivyodhamiria katika kazi yangu ya ukocha, nataka kuifundisha Taifa Stars ndoto ambazo naamini siku moja zitafanikiwa,” anasema Macho.

Amesema, kwa sababu sasa ana leseni C, anachotaka kufanya ni kuongeza elimu yake ya ukocha zaidi na zaidi ili aweze kufikia vigezo vinavyotakiwa kwa kusoma leseni B na A.

“Nimeshindwa kuendelea na masomo ya ukocha kutokana na kozi hizo kusimama kwa muda, zitakapoanza nitakwenda kuongeza elimu yangu hiyo.”

VIUNGO WAKE BORA

Macho ambaye aliweza kucheza nafasi zote za kiungo na ushambuliaji, anasema nafasi hiyo kwa sasa haina watu wengi wenye vipaji vikubwa nchini na waliopo wengi upungufu mkubwa.

“Wakati nacheza mimi nilikuwa na uwezo wa kuchezesha timu, nafunga na hata kuzuia, nazunguka uwanja mzima kuhakikisha timu yangu inafanikiwa, lakini vijana wa sasa hawako hivyo siyo wapambanaji,” anasema Macho.

“Wengi wao hawajitumi wanacheza ilimradi tu. Kwa Tanzania nilikuwa namtegemea zaidi Jonas Mkude wa Simba afike mbali, lakini yeye naye kwa sasa imekuwa kinyume. Hayuko siriazi kwa sababu hata anapopoteza mpira huoni kama anajuta, hapambani vile uone kweli anapambana.

“Mudathir Yahya wa Azam FC kidogo anajaribu, lakini kwa upande wake ana upungufu mwingi, anatakiwa kuboresha namna yake ya uchezaji wa kudhibiti maeneo, yaani wanaposhambulia afanye nini na wanapokuwa hawana mpira afanye nini.”

AMPONGEZA MO DEWJI

“Mo Dewji ni mtu wa mpira namjua, akiamua lake hamuwezi kushindwa hasa kutokana na uhamasishaji wake, nampongeza sana,” anasema Macho akisisitiza hata hivyo kuna mambo mengine ambayo Simba wanatakiwa kuweka sawa.

Usikose sehemu ya mwisho ya makala haya kwenye Mwanaspoti kesho Jumatano uone sababu zinazomfanya atake kuongeza mke wa tatu.