Yupo Ozil mmoja tu mjue!

LONDON, ENGLAND. MAISHA ndivyo yalivyo. Misimu minane ya supastaa Mesut Ozil kwenye kikosi cha Arsenal imepita kwenye zama nyingi, kupanda na kushuka huku msimu huu mambo yakiwa magumu zaidi, akipigwa chini kwenye kikosi cha Ligi Kuu England na Europa League chini ya kocha Mikel Arteta.

Wakati anatua Emirates mwaka 2013 akitokea Real Madrid, usajili wake ulionekana kuwa wa kibabe zaidi kuwahi kufanywa na Arsenal kipindi hicho ilipokuwa chini ya kocha Arsene Wenger. Wachezaji kibao waliokuwa wakicheza pamoja na Ozil huko Real Madrid, ikiwamo Cristiano Ronaldo, hawakufarahia kuuzwa kwa Mjerumani huyo kwenda Arsenal.

Lakini, kwa sasa akiwa mchezaji aliyedumu muda mrefu kwenye kikosi cha Arsenal na kulipwa mshahara mkubwa, Ozil hapewi tena thamani yake na hivyo anawekwa tu benchi akisubiri mkataba wake ufike mwisho mwakani.

Mavitu ya Ozil kwenye kikosi cha Arsenal ni babu kubwa, alipiga asisti kwenye mechi yake ya kwanza tu kwenye kikosi hicho, wakati alipotengeneza bao matata la straika Olivier Giroud kwenye ushindi wa 3-1 dhidi ya Sunderland. Kocha Jose Mourinho aligoma kumpeleka kwa mkopo Demba Ba kipindi hicho akiwa Chelsea kwa sababu tu Wenger alikuwa amenasa huduma ya Ozil, aliogopa kombinesheni yao ingekuwa balaa zito kwenye ligi. Uzio wa Ozil kwenye kikosi cha Arsenal ulimaliza ukame wa mataji, ambapo staa huyo aliisaidia Arsenal kubeba taji lake la kwanza la Kombe la FA baada ya kusubiri kwa miaka tisa, waliposhinda 3-2 kwenye fainali dhidi ya Hull City mwaka 2014. Hilo lilikuwa taji la kwanza kwa Arsenal baada ya kusubiri kwa miaka mingi kabla ya kubeba msimu uliofuatia wakitamba na huduma ya Ozil kwenye kikosi chao.

Ozil ni hatari pia kwa kuwatengenezea pasi za mabao wenzake, ambapo kwenye kikosi cha Arsenal ameasisti mara 77 katika mechi 254 alizocheza kwenye michuano yote.

Kiungo huyo fundi wa mpira aliweka rekodi ya kuwa staa wa kwanza kufikisha asisti 50 haraka zaidi kwenye Ligi Kuu England, kabla ya rekodi yake hiyo kuvunjwa na mkali wa Manchester City, Kevin de Bruyne. Hata hivyo, Ozil anashikiria rekodi ya kupiga asisti mfululizo kwenye mechi nyingi za Ligi Kuu England, akifanya hivyo kwenye mechi saba mwaka 2015.