Yanga yakomaa na mastraika wanne

Sunday May 31 2020

KUNA watu wanne wanakiona chamoto kwelikweli kwenye mazoezi ya Yanga tangu yaanze chini ya Kocha msaidizi, Boniface Mkwasa.

Katika mazoezi hayo ambayo yanaendelea kwenye Uwanja wa Chuo cha Sheria Jijini Dar es Salaam, Mkwassa amebaini kuna tatizo kwa wachezaji hao wanne ambao ni David Molinga, Ditram Nchimbi, Tariq Seif na Yikpe Gnamien.

Tizi hilo ambalo hupigwa kila siku jioni, kocha huyo amekuwa akisimamia mazoezi ya fiziki ili kuwajenga wachezaji wote kwa ujumla sambamba na mbio na mbinu za kiuchezaji na mara kadhaa huwagawa kwa makundi.

Lakini mastraika hao amewafungia kazi kuhakikisha wanarudisha kasi yao kwani amebaini walikuwa hawachezei mpira wakati wa likizo ya corona.

Molinga ndiye kinara wa mabao katika kikosi cha Yanga mpaka sasa kwenye Ligi Kuu Bara, amefunga mabao nane.

Katika mazoezi ya siku mbili mfululizo, Molinga alionekana kutokuwa na amani kwani muda wote alikuwa ni mchezaji wa kuongea pembeni na kutofurahia mazoezi kama ilivyo kuwa kwa wachezaji wengine.

Advertisement

Molinga juzi jioni alikuwa akikabwa na Kelvin Yondani na hakupiga shuti hata moja katika mazoezi hayo yaliyotumia dakika 30, na muda wote alikuwa hana madhara.

Nchimbi yeye, katika mazoezi hayo ndio straika pekee ambaye alionyesha uwezo pengine kuliko wote kwani alipiga shuti moja tu ambao liligonga mwamba.

Ditram alitumia nguvu nyingi na kushindana na mabeki lakini umiliki wa mpira ulimpotea.

Alionekana kuwa fiti kimbinu kuliko mastraika wengine.

Tariq tangu matizi yaanze ameonyesha uwezo wa mbio na kutafuta mpira katika maeneo mengi ya uwanja ingawa bado anakosa utulivu.

Juzi Tariq alipangwa timu moja na Nchimbi lakini alikosa nafasi nne za wazi akiwa uso kwa uso na kipa Ramadhani Kabwili.

Yikpe ambaye ameifungia Yanga mabao mawili katika ligi na jingine kwenye Kombe la Shirikisho (FA), mazoezini bado alionekana mzito ingawa alikuwa akilazimisha kupiga chenga na kutumia mwili wake vizuri lakini mabeki walimzidi ujanja.

Alicheza sambamba na Molinga lakini alipoteza mipira, hakuwa na maelewano mazuri na mwenzie.

Kocha anasema shida kubwa ambayo ameiona kwa wachezaji hao walikuwa wanafanya zaidi mazoezi ya nguvu kuliko kuchezea mpira kipindi chote ambacho ligi ilikuwa imesimama.

“Hilo ndio tatizo la kwanza ambalo nimeliona kwa wachezaji wengi wa kikosi changu ndio maana wakiwa na mpira katika miguu yao ni rahisi kupoteza kuliko kuwa salama,” alisema.

“Ingawa si wachezaji wote wapo na shida hiyo, ila tunakwenda kulifanyia kazi hili na tuna imani kwa muda mfupi kabla ya ligi kuanza mambo yote ya kiufundi yatakuwa sawa,” alisema Mkwasa ambaye anaendelea kuwajibika mpaka Mbelgiji Luc Eymael atakaporejea Bongo.

WAJIFUA DK.130

Mkwasa juzi jioni pia aliwapa wachezaji wake mazoezi kwa dakika 130 bila kupumzika na kuwaachia dakika tano za kunywa maji.

Mwanaspoti lilishuhudia wachezaji wa timu hiyo wakihenyeka kuanzia saa 10:15 jioni hadi saa 12:30.

Mkwasa alianza kuwapa wachezaji wake mazoezi mepesi ya viungo kwa nusu saa kisha akawataka kukimbia kwa kasi kutoka eneo moja la goli hadi lingine huku akiwahesabia moja hadi 10.

Zoezi hilo lilidumu kwa dakika 20 kisha kuwaruhusu kunywa maji kwa dakika mbili na kuwataka kurejea uwanjani.

Baada ya hapo Mkwasa aliwapangia koni ndefu na kumtaka kila mchezaji kuruka bila kuangusha, zoezi ambalo wachezaji wote walilimudu na akawapa breki ya kunywa maji kwa dakika tatu na waliporejea aligawa vikosi viwili kikapigwa saa nzima na kisha saa 12:30 giza likiwa limeanza kutanda akafunga mazoezi.

Mkwasa alisema; “Walikuwa wanafanya mazoezi nyumbani lakini huwezi kujua walikuwa wanafanya kwa kiwango gani hivyo lazima wapate mazoezi ya nguvu ili kuwaweka sawa.

“Ndio maana nimewapa mazoezi kwa muda mrefu na nitakuwa nafanya hivyo mpaka pale nitakapohakikisha timu nzima inakuwa fiti kwa sababu hata ukiangalia muda ni mchache kabla ya ligi kurejea hivyo hakuna kuremba lazima wafanye mazoezi ya nguvu,”alisema Mkwasa.

IMEANDIKWA NA OLIVER ALBERT, THOBIAS SEBASTIAN NA THOMAS NG’ITU

Advertisement