Yanga kuingia mkataba na La Liga ya Hispania

Sunday May 31 2020

 

By MWANDISHI WETU

SAFARI ya Yanga kutimiza ndoto ya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wake, inaanza leo wakati klabu hiyo itakaposaini mkataba na Bodi ya Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) kwa ajili ya kuwaongoza katika mchakato huo.

Inaelezwa kwamba mkataba huo utaifanya Yanga iwe kama Seville iliyowahi kuja nchini na kucheza na Simba na kushinda mechi hiyo ya kirafiki kwa mabao 5-4.

Hafla ya utilianaji saini wa mkataba huo baina ya La Liga na Yanga itafanyika leo jijini Dar es Salaam katika Hoteli ya Serena kuanzia kuanzia saa 1:00 usiku.

Ofisa Uhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz alisema mkataba huo utasainiwa ukiishirikisha pia kampuni ya GSM ambayo ndio itakayogharamia mchakato huo.

“Moja kati ya azma za mwenyekiti (Dk Mshindo Msolla) tangu anachukua nafasi, shabaha yake namba tatu kama sio namba mbili ilikuwa ni kufanya mabadiliko ya kuitoa klabu ilipo katika uendeshaji tegemezi kwenda kuwa tegemewa. Yaani ijitegemee,” alisema Nugaz.

“Tunakwenda kutia sahihi, uanzishwaji kamili wa mchakato sahihi wa kwenda na wakati husika.

Advertisement

“Ni mkataba baina ya Yanga na La Liga. Ukisimamiwa na ukifadhiliwa na GSM. Sio GSM ambaye ndiye anafanya mabadiliko. Mabadiliko yatafanywa na Yanga.” Nugaz alisema uamuzi wa kuishirikisha La Liga umetokana na uzoefu walionao kutokana na uendeshaji na mafanikio ya soka la Hispania.

Naye Katibu Mkuu wa Yanga, David Ruhago alisema ni mwanzo wa kuipeleka klabu hiyo kwenye mafanikio.

“Njia pekee ya kujikwamua na kuwa na timu ya ushindani ni kuwa na mfumo sahihi wa kisasa ili kuepuka kuwa tegemezi. Wanayanga wenzangu tushikamane na tuungane kwenye hili,” alisema.

Advertisement