Yajayo yanafurahisha

Friday August 10 2018

 

By OLIPA ASSA

KAMA wewe ni shabiki wa Simba basi jiandae tu kwa sasa, Kaimu Rais wa Wekundu wa Msimbazi hao, Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema katika msimu unaotarajia kuanza hivi karibuni wanachama, mashabiki na wapenzi wa Simba hawatakaukiwa na tabasamu kwa mambo mazuri yajayo.

Kiongozi huyo amesema wachezaji wao wanaonyesha kiwango cha juu wakiwa wamekaa wiki mbili tu na kocha wao mpya Mbelgiji Patrick Aussems, jambo alilodai wanaamini mbele wataona vitu vikubwa vya kiufundi.

“Umefika wakati wa mashabiki wa Simba kusahau machungu yote yaliyowahi kutokea kipindi cha nyuma, ni kwa sababu sasa tuna timu nzuri na kikosi kipana,” alisema.

“Mfano mzuri ni huu, kocha amekaa na timu wiki mbili tu, lakini wachezaji wanaonekana wanafanya vitu vikubwa uwanjani.

“Kitu kimoja tu mashabiki wanatakiwa kuelewa kwamba kutoka sare na Asante Kotoko ni kwa vile timu imetoka kwenye maandalizi ya msimu mpya, pia wapinzani wetu nao ni wazuri na wana hadhi kwa uwezo mkubwa walionao.”

Try Again aliwataka mashabiki wa Simba kuacha tabia ya kumshinikiza kocha kumpanga mchezaji wanayemtaka, akidai hawajui nini kipo nyuma ya pazia ama mipango ya kocha ni ipi.

“Kwa Simba hii inahitaji mabadiliko makubwa, kwanza mchezaji asipopangwa wajue wazi kocha ana sababu zake, inawezekana ikawa majeraha, kuumwa kwa ghafla, ama nidhamu mbovu, hizo ni kati ya sababu ambazo kocha anaamua kumweka mchezaji benchi.

“Kila kocha anahitaji mafanikio ndani ya klabu, hivyo haiingi akilini kumuacha mchezaji nje kwa makusudi wakati anajua atamsaidia kupata matokeo, tubadilike na tufanye mambo kimataifa.”

Kuhusu Simba Day, alisema ina mabadiliko makubwa kutokana na walivyoifanya kwa mpangilio mzuri, mwitiko wa mashabiki, kuleta timu bora na wasanii wakali.

Advertisement