Wote Wapo sokoni

WAKATI mashabiki wakingoja burudani ya michezo ya Ligi Kuu kurejea Juni 13, wachezaji na viongozi nao wanangoja msimu umalizike na zoezi la usajili lianze ili kuboresha vikosi vyao.

Wachezaji nao ndio muda wao wa kupiga pesa katika usajili huku asilimia kubwa ya washambulia wanaotikisha nyavu kwenye timu hasa wazawa, kandarasi zao nazo zinakwisha. Wapo sokoni.

Kama sio corona Ligi Kuu pamoja na Kombe la FA bingwa tayari angekuwa amepatikana na kuanza kujiandaa na msimu ujao kwaajili ya kuwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa.

Reliants Lusajo wa Namungo FC mwenye mabao 11 ambaye ni kinara wa kufunga kwenye timu hiyo na mfungaji bora msimu uliopita Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa mabao yake 15 naye yupo sokoni.

Lusajo tayari mkataba wake umekwisha lakini kutokana na mabadiliko yaliyosababishwa na janga la corona anangoja kumaliza michezo ya msimu ili mambo yawe sawa kwake.

Licha ya viongozi wa Namungo kuwa tayari kumpa kandarasi mpya lakini nyota huyo amegoma hadi msimu utakapokwisha.

Yusuph Mhilu (Kagera Sugar) mwenye mabao 11 alitua hapo kwa mkataba wa mwaka mmoja kutoka Ndanda FC na mkataba wake unaelekea ukingoni hajawa tayari kuongeza mkataba akisubiri ligi imalizike kwanza.

Daruweshi Saliboko mwenye mabao nane tayari katingisha kiberiti kwa viongozi wa timu ya Lipuli FC kuwa hataweza kurejea kutokana na madai yake tangu aliposajiliwa.

Saliboko alisema anaidai Lipuli Sh 6,600,000), fedha za mshahara anazoeleza kuwadai ni Tsh 2,400,000 ambazo ni miezi sita, miezi mitatu msimu uliopita na miezi mitatu msimu huu na fedha za usajili Sh4,200,000).

Waziri Junior kinara wa mabao Mbao FC akiwa amefunga mabao saba naye atakuwa sokoni baada ya dirisha kubwa la usajili kufunguliwa kama ilivyo kwa Sixtus Sabilo wa Polisi Tanzania mwenye mabao saba.

Marcel Kaheza anayekipia Polisi Tanzania kwa mkopo kutoka Simba ana mabao sita naye yupo sokoni na tayari ameeleza hayupo tayari kurudi Simba.

“Hakuna mazungumzo yoyote hadi sasa kati yangu na uongozi wa Simba licha ya mkataba wangu kuelekea mwisho, ila Polisi nimeanza nao mazungumzo. ili kama vipi nisalie hapa,” alisema Kaheza na kuongeza;

“Kusema kama siwezi kurudi Simba inawezekana ila wakinihitaji na kukamilisha yale ninayoyataka ikiwemo maslahi yangu binafsi nitarudi.”

Mathias Mdamu wa Mwadui FC mwenye mabao matano kwa sasa mkataba wake umemalizika na anachongojea ni kumaliza michezo ya mwisho ya kufunga msimu, huku uongozi nao ukimpa mkono wa kwaheri.

“Hakuna mtu aliyekuwa anamjua Mdamu kabla hajawafungwa Simba, lakini anacheza hapa kutokana na uzoefu aliokuwa nao, kuhusu kuondoka hilo halina wasiwasi kwetu, anaweza kuondoka tu” alisema Katibu wa timu hiyo, Ramadhan Kilao.