Waziri Jr ajihakikishia ushindi

Muktasari:

Junior ndio kinara wa mabao katika klabu ya Mbao akiwa na magoli sita mpaka hivi sasa.

BAADA ya kuiongoza Mbao FC kuifunga Singida Utd  mabao 3-1 katika mchezo wao uliopita wa Ligi Kuu Bara, Nahodha wa timu hiyo Waziri Junior ametamba kuiongoza timu hiyo kuibuka na ushindi leo Jumamosi dhidi ya Mwadui FC mchezo utakaochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.
Junior alisema wana morali kubwa kuhakikisha wanapata matokeo mazuri ili kuisaidia timu kuzidi kusogea nafasi za juu na kuepukana na rungu la kushuka daraja.
"Mechi ya leo tunahitaji ushindi na wachezaji wote morali yetu ipo hivyo, ushindi muhimu kwasababu tutakuwa angalau tuna uhakika wa kuendelea kubaki Ligi Kuu japo ligi haijaisha," alisema.
Mshambuliaji huyo aliongeza kuwa ushindi wa leo unakuwa na maana kubwa kwani mechi zijazo wataenda kucheza ugenini.
"Baada ya mechi hii tutaenda kucheza ugenini na Ruvu pamoja na Yanga, mechi za ugenini unaweka asilimia 40 ya ushindi kwahiyo inatubidi tutumie uwanja wetu wa nyumbani vizuri," alisema.
Mbao inashika nafasi ya 16 wakiwa na pointi 22 katika michezo 23 waliyocheza kabla ya mchezo wao wa leo jioni.