Tshishimbi : Simba watajuta, mbona ubingwa nasi tunautaka

Muktasari:

Pia alifichua juu ya mabadiliko ya benchi la ufundi la Yanga sambamba namna usajili uliofanywa Jangwani, na leo Alhamisi mkali huyo anaendelea kuzungumzia mambo mengine kuhusu maisha yake tangu ametua hapa nchini Agosti 2017, pamoja na changamoto alizokutana nazo katika kikosi hicho ambacho jana usiku kilikuwa kikivaana na Lipuli, huku akiichimba mkwara juu ya mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la FA...Kivipi? Endelea naye!

KATIKA toleo la juzi Jumanne, tuliona namna Nahodha wa Yanga, Mkongomani Papy Kabamba Tshishimbi aliyetembelea makao makuu ya Mwananchi Communications Limited, yaliyopo Tabata Dar es Salaam, alivyotoboa juu ya kucheza kwake kwenye kiwango cha juu anapocheza mechi kubwa dhidi ya Simba na Azam.

Pia alifichua juu ya mabadiliko ya benchi la ufundi la Yanga sambamba namna usajili uliofanywa Jangwani, na leo Alhamisi mkali huyo anaendelea kuzungumzia mambo mengine kuhusu maisha yake tangu ametua hapa nchini Agosti 2017, pamoja na changamoto alizokutana nazo katika kikosi hicho ambacho jana usiku kilikuwa kikivaana na Lipuli, huku akiichimba mkwara juu ya mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la FA...Kivipi? Endelea naye!

UBINGWA

Kikosi cha Yanga kwa sasa kipo katika michuano miwili - kwa maana ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (ASFC), na kati ya hayo mawili kama wakifanikiwa kuchukua ubingwa mojawapo au yote watashiriki mashindano ya kimataifa msimu ujao.

Tshishimbi anasema kwa ambavyo kikosi chao kimezidi kuimarika baada ya kufanya usajili kwenye dirisha dogo na maboresho ya benchi la ufundi, wana uwezo wa kushindana na timu zote zilizo katika mashindano hayo na wakatwaa ubingwa.

“Bado tuna nguvu ya kushindana katika ligi na Simba ambao wanaongoza na tukachukua ubingwa, hata sisi tunaweza kuwa bora dhidi ya timu ambazo tunakutana nazo katika FA na tukatwaa ubingwa wa kombe hilo, hivyo wapinzani wetu wasijidanganye na kuamini kazi imeisha,” anasema.

MZEE WA PAMBA

Tshishimbi kama ilivyo kwa Wakongomani wenzake anakiri kuwa miongoni mwa vitu anavyopenda katika maisha yake tangu akiwa mdogo ni kuonekana nadhifu hata kama akiwa hana fedha mfukoni, kwani anaamini akiwa hivyo ni rahisi kuonekana katika mambo mengi ya kimsingi kuliko unadhifu ukimshinda.

“Kiukweli napenda sana kupiga pamba na kuwa blingbling muda wote, ndio maana nachukua muda kuangalia nguo gani nikivaa na nyingine nakuwa na muonekano mzuri na hata ukiniangalia katika shughuli zangu za kila siku muonekano wangu upo nadhifu kutokana na nguo ambazo navaa,” anasema.

“Natumia muda kuangalia nguo za kuvaa wala sina mtu yeyote ambaye ananichagulia nguo ya kuvaa kwani ni mimi mwenyewe huwa najua tukio ambalo nakwenda kukutana nalo mbele yangu, na navaa nguo ambayo inalingana na hali hiyo.”

HATA BUKU FRESHI

Tshishimbi anasema katika kutafuta nguo za kuvaa zile ambazo anazipenda sio kama ananunua zile za gharama tu, bali hata kama akikutana na pamba inayouzwa buku (Sh 1,000) anaichukua na anakwenda kuvaa na muonekano wake unakuwa kama kawa.

“Wala sioni noma kwangu hata kama nikikuta nguo yoyote au kiatu kinauzwa buku au bei cha chini naenda kununua na nikija kuvaa unaweza kusema nilinunua kwa bei ya juu, kumbe ni buku tu. Kwa hiyo hilo la kuvaa vitu vya gharama kwangu si mara kwa mara,” anasema Tshishimbi.

VIATU VINGI

“Kama ambavyo nimeeleza hapo awali huwa napenda kuvaa, basi katika kabati langu nina nguo nyingi pamoja na vitu ambavyo vingine sivikumbuki kwamba nilivivaa siku nyingi nyuma na hata idadi ya nguo na vitu ambavyo ninavyo siwezi kuvikumbuka pia kwa maana ni nyingi mno.”

Anasema, “nimekuwa na viatu na nguo nyingi kutokana kila mahala au eneo nakwend nikiwa na timu au mwenyewe mara nyingi pesa yangu huwa nakwenda kuitumia katika manunuzi ya nguo na viatu ambavyo navaa mara kwa mara na vingine nashindwa kuvirudia maana ni vingi.”

KUSEPA YANGA

Tshishimbi anasema sio kama anacheza katika kikosi cha Yanga basi muda wote atakuwa na mawazo ya kudumu katika timu hiyo, bali kama mchezaji anafikiria malengo mengine mengi ya mbele zaidi ambayo kila binadamu anakuwa nayo katika ndoto za kuzitimiza maishani mwake.

“Nina malengo ya kwenda kucheza soka mbele zaidi, kwa hiyo muda muafaka wa kuondoka hapa Yanga ukifika nitawafahamisha hilo, lakini wakati huu bado nguvu na akili yangu inaifikiria hapa nilipo,” anasema.

Tshishimbi anasema: “Bado nina mkataba ambao natakiwa kuupa heshima na kuutumikia kwa uwezo wangu wote.”

MASHABIKI YANGA

Mechi ya kwanza ya Kocha mpya wa Yanga wa sasa, Mbelgiji Luc Eymael ilikuwa dhidi ya Kagera Sugar ambayo walichezea kichapo cha mabao 3-0 wakiwa katika Uwanja wa Uhuru, na mara ya baada ya kumalizika kwa mchezo huo mashabiki wa Yanga walipanga msururu na kuanza kuwapigia makofi wachezaji wao walipokuwa wanatoka uwanjani.

Tshishimbi anasema katika mechi hiyo hakucheza, lakini anawapa ujumbe wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kuwa alifanya jambo kubwa na bora ambalo liliwafurahisha wachezaji wote na kuwapa moyo wa kwenda kupambana zaidi katika mechi zilizofuata ili kupata matokeo mazuri.

“Tukio lile ambalo walifanya mashabiki wa timu yetu ya Wananchi lilitugusa mno wachezaji na mpaka benchi la ufundi kuwa kweli wenye timu wanaipenda, na wanatambua mchango wetu kama nasi tunavyopigana timu,” anasema Tshishimbi ambaye alijiunga na Yanga Agosti 2017.

“Licha ya kupoteza lilikuwa jambo kubwa kwetu kupigiwa makofi na mashabiki huku tukitoka kupoteza mchezo.”

EYMAEL AMSHTUA

Tshishimbi anafichua kuwa, tangu Yanga iwe chini ya Kocha Eymael aliyechukua mikoba ya kuinoa timu hiyo kutoka kwa kocha wa muda Boniface Mkwasa, ambaye ni msaidizi wake kwa sasa, kuna mabadiliko makubwa yanayoifanya timu ijitofautishe licha ya nyota kuwa ni walewale.

Anasema tangu kocha huyo amekuja amejenga utamaduni wa kutoangalia majina makubwa ya wachezaji, bali anaangalia uwezo wa kila mchezaji ambaye anajituma na kutimiza majukumu yake uwanjani na hilo limefanya wachezaji wa Yanga kuamka na kupambana ili kujihakikishia namba tofauti na zamani.

“Aaaahhh!! Huyu Eymael amewashtua wachezaji wengi katika kikosi chetu kwani haangalii sura au jina la mchezaji, bali anataka wale ambao wanafanya kazi katika mazoezi kulingana na yale maelekezo ambayo huwa anayatoa kutokana na mbinu za mechi husika, na hii imeongeza ushindani ndani ya timu.”