Tammy Abraham hakomi kupiga penalti Chelsea

Saturday August 17 2019

 

LONDON, ENGLAND . STRAIKA wa Chelsea, Tammy Abraham amesema ataendelea kupiga penalti za timu hiyo licha ya sasa kukumbana na wakati mgumu wa meseji za kutukanwa na kubaguliwa kutokana na rangi ya ngozi yake baada ya kukosa mkwaju wake dhidi ya Liverpool .
Fowadi huyo amekuwa akitumiwa meseji nyingi za vitisho na za kibaguzi kwenye ukurasa wake wa Twitter baada ya kukosa mkwaju wake wa penalti kwenye mechi ya Uefa Super Cup Jumatano iliyopita, ambapo Chelsea walipoteza kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 2-2 katika dakika 120.
Wasimamizi wa kupinga ubaguzi Kick It Out wamethibitisha meseji hizo kumlenga Abraham na kusema ni vitu vya kujiunga kwa watu kuendelea kukumbatia ubaguzi katika zama hizi.
“Tupo pamoja na Tammy na tunapinga haya mambo yote yanayofanywa kwenye Twitter na mitandao mingine ya kijamii kuacha unyanyasaji huu. Hatua zichukuliwe sasa na ufahamike kama jambo hilo linakwenda kukomeshwa lini," ilibainisha taarifa hilo ya Kick It Out.
Abraham amekiri kuhuzunishwa kwa kukosa penalti hiyo, lakini alisema hawezi kujiweka pembeni ikipatikana nyingine atapiga.
“Niliwahi kufunga nyingine chache. Kwa bahati mbaya nimekosa penalti muhimu sana kwa Chelsea. Wanasema hata wanasoka mahiri wanakosa penalti, nitaendelea kupiga," alisema.
Kocha Frank Lampard amempa sapoti kubwa mchezaji wake sawa na ilivyo kwa uongozi wa klabu kuhakikisha wanamwaandaa vyema kisaikolojia kinda wao huyo na kumuunga mkono katika kipindi hiki cha kuandamwa na mashabiki wakorofi.
“Nilimwambia asiwe na wasiwasi,” alisema Lampard baada ya mechi. “Kitu muhimu ni kwamba anajiamini na kuamua kwenda kupiga penalti ya tano, hilo limenifurahisha sana. Hata mimi iliwahi kunitokea, yeyote anaweza kukosa penalti, lakini ninachotaka ni kujiamini kwa mchezaji kama yeye mdogo.”

Advertisement