Straika mpya Azam anataka namba ya Ngoma

Muktasari:

 Khamisi ni mchezaji wa nne kusajiliwa katika kikosi cha Azam FC ambacho hadi sasa baada ya awali kuwasainisha Idd Seleman, Emmanuel Mvuyekure na Seleman Ndikumana.

MSHAMBULIAJI mpya wa Azam FC,  Kassim Khamis amesema hana hofu na mchezaji yoyote ndani ya kikiso hicho kwani anachokiamini ni kuwemo kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Etienne Ndayiragije.
Khamis anacheza nafasi moja na Obrey Chirwa, Donald Ngoma, Seleman Ndukumana, Idd Seleman 'Nado' na Emmanuel Mvuyekure ambapo atapaswa kupambana ili kupata namba ambapo Ngoma ndiye mara nyingi alikuwa akicheza kikosi cha kwanza huku akimaliza msimu akiwa na mabao 11.
Msimu uliopita Chirwa alimaliza akiwa na magoli matatu wakati Nado, Ndikumana na Mvuyekure nao ni usajili mpya ndani ya Azam.
Khamis amesaini mkataba wa miaka miwili akitokea Kagera Sugar akiwa ni miongoni mwa nyota waliopambana kuhakikisha wanaibakiza timu hiyo Ligi Kuu baada ya kuwafunga Pamba bao 2-0 mechi ya mchujo.
Amesema hawezi kuogopa changamoto mpya katika timu yoyote anayopata nafasi ya kusajiliwa huku akitolea mfano alipotoka Prisons kwenda Kagera Sugar kwamba alipambana na kujimini kuhakikisha anapata namba kikosi cha kwanza.
"Nakumbuka niliposajiliwa Kagera dirisha dogo nilikosa michezo miwili kutokana na kukosa kibali cha kuniruhusu kuanza kuitumikia timu hiyo, nilikaa jukwaani ambapo nilikuwa nawasoma wachezaji wanaocheza nafasi ninayocheza,"
"Nilikuwa jukwaani na mchezaji wa umri wa miaka 20 wa timu ya Kagera nilimwambia unaangalia huu mchezo kwa makini kuna mchezaji ana namba yangu hapo nikipata kibali atanipisha hakuamini, mchezo wangu wa kwanza nikiwa Kagera ulikuwa ni dhidi ya Mwadui FC nilicheza dakika 45 za kipindi cha kwanza na kutolewa tulifungwa mabao 4-0,"
"Mchezo wangu wa pili ilikuwa ni dhidi ya Afrikan Lyon nilifunga mabao mawili na huo mchezo ndo ulifungua akaunti ya mabao kwani baada ya mchezo huo pia mchezo uliofuata sikumbuki tulicheza na timu gani nilifunga tena," anasema Khamis aliyemaliza msimu akiwa na mabao saba.