Simba, Yanga kimenuka

YANGA imeanza mazungumzo rasmi na wakala wa straika, Mburkina Fasso, Yacouba Sogne ambaye yuko kwenye rada ya Simba.

Mchezaji huyo mwenye rasta kwa sasa amepumzika kwao baada ya kugoma kuongeza mkataba na Asante Kotoko hivi karibuni kwa ishu za kimasilahi.

Simba walishaanza mazungumzo na mchezaji huyo na yupo kwenye malengo yao lakini wiki iliyopita, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba aliiambia Mwanaspoti kuna sehemu wanasita.

“Huyo mchezaji wamekuja mawakala kibao kila mmoja anasema ni wakala wake anamsimamia ndio maana tumeamua kutulia kidogo,” alisema Senzo.

Lakini habari za uhakika ambazo jana Mwanaspoti imezipata kwa Yanga na Kotoko, mchezaji huyo kuna wakala wake mmoja yuko bize na GSM na huenda dili hilo likafikia pazuri muda wowote.

Habari zinasema GSM wamepiga mpaka simu Kotoko kuulizia mchezaji huyo na wakaambiwa mkataba wake umemalizika na sasa wanazungumza na wakala wake anayemsimamia ingawa waligoma kusema ni nani na yuko nchini gani.

Mwanaspoti ilimuuliza kigogo huyo wa Yanga kama wanaelewa Simba wamekumbana na ishu ya mawakala wa mchezaji huyo, lakini akasisitiza wanajua wanachokifanya na mambo yao yanakwenda kimyakimya.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imejiridhisha nazo ni mzigo ambao Yacouba ameutaka ili atue Jangwani msimu ujao mabosi wa GSM na Yanga wamewapa jibu hakuna kinachoshindikana dili itamalizwa ingawa wamegoma kutaja kiasi walichokubaliana.

Hatua ya Yanga kuingilia dili hilo, inaweza kuamsha vita mpya kwani wakala wa mchezaji huyo wanaangalia mshiko tu.

“Yacouba mbona Yanga ndio wanazungumza na wanaomsimamia tunajua kila kitu kinavyokwenda,” alisema mmoja wa mabosi wa Kotoko ingawa Mwanaspoti linajua Simba hawakuwahusisha Kotoko kwa vile wanajua mkataba wa mchezaji umekwisha na hawana chao.

Mchezaji huyo ambaye amekuwa akihusishwa pia na ZESCO ya Zambia na Orlando Pirates ya Afrika Kusini ameliambia gazeti moja la Ghana hana presha.

“Wakala wangu kuna timu anazungumza nazo baada ya hii corona kumalizika nitaambiwa ni wapi nakwenda.

“Kwa sasa yanasemwa mengi lakini nimetulia kwanza,” alisema mchezaji huyo ambaye inasemekana akili yake ipo zaidi Barani Asia lakini anataka kusaini mkataba wa muda mfupi Simba au Yanga kwa yoyote atakayekuwa na kisu kirefu.

Habari zinasema wakala wa mchezaji huyo anadai thamani yake ni Dola 150,000 sawa na zaidi ya Sh300 milioni lakini Yanga na Simba bado wanaendelea kumchekecha na kuna dalili ya kushuka mpaka Sh100 milioni.

Matajiri wa Yanga na Simba wamepania kusuka upya vikosi hivyo, huku Kocha wa Yanga, Luc Eymael akitaka wachezaji takribani saba.

Senzo amekuwa akisisitiza kwamba watasajili wachezaji wa maana wa gharama kubwa wasiozidi wanne kwani timu yao bado ni imara, wanahitaji kuwa nayo muda mrefu na inahitaji mabadiliko madogo ya kimsingi mbele, kati na nyuma.