Saul kaishika pazuri Man U

Muktasari:

Hata hivyo suala la kumpata Saul litategemea na Pogba kama ataondoka kwenye kikosi hicho ambapo kwa sasa amekuwa akihusishwa na vigogo Real Madrid na Juventus.

MADRID, HISPANIA . NDO hivyo. Manchester United inafahamu kwamba inakabiliwa na wakati mgumu katika kutimiza ndoto zao za kumnasa kiungo wa Atletico Madrid, Saul Niguez.
Staa huyo amekuwa akitazamwa kama mtu wa kwenda kuongeza makali kwenye kiungo ya Man United hasa wakati Paul Pogba atakapofungasha virago vyake na kuondoka.
Lakini, kwa mujibu wa AS, Atletico wameripotiwa kwamba watahitaji kulipwa Pauni 132 milioni kama kinavyoelezwa kipengele kilichowekwa kwenye mkataba wa mchezaji huyo ambaye ameibukia kutokea kwenye akademia ya klabu hiyo.
Kipengele hicho kilichomokwa kwenye mkataba wa miaka tisa wakati aliposajili mwaka 2017. Kiwango hicho cha pesa ni kikubwa kuliko ilichotoa Man United kunasa saini ya Pogba, Pauni 89 milioni kutoka Juventus mwaka 2016.
Kama pesa hiyo italipwa basi Saul atakuwa kiungo ghali zaidi kwenye kikosi ya Man United. Hata hivyo, wakali hao wa Old Trafford wameripotiwa kwamba hawatakuwa tayari kutoa pesa zaidi ya Pauni 70 milioni kunasa saini.
Hata hivyo suala la kumpata Saul litategemea na Pogba kama ataondoka kwenye kikosi hicho ambapo kwa sasa amekuwa akihusishwa na vigogo Real Madrid na Juventus.
Beki wa zamani wa Man United, Rio Ferdinand alizungumzia ishu ya Saul na kusema: "Sitaki Pogba aondoka, lakini nataka Saul Niguez asajiliwe. Ni mchezaji wa daraja la juu. Ni mchezaji mkubwa."
Saul amecheza mechi 286 kwenye kikosi cha Atletico, akifunga mbao 38 na kuasisti 18.