Ribery anatajwa Sheffield United

Friday June 14 2019

 

LONDON, ENGLAND.DUNIANI kuna mambo wanasema. Sheffield United baada ya kupanda daraja na kucheza Ligi Kuu England kuanzia msimu ujao, wameripotiwa kuwa na mpango wa kufanya usajili wa kuwaduwaza wengi, wakimtaka supastaa Franck Ribery.
Staa huyo Mfaransa, Ribery kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kuachana na Bayern Munich mwishoni mwa msimu uliomalizika, mahali ambako alidumu kwa miaka 12 na kubeba mataji 22.
Ribery, mwenye umri wa miaka 36, amecheza mechi 81 pia kwenye timu yake ya taifa ya Ufaransa, ameripotiwa kwamba huenda akatia nanga huko kwenye Ligi Kuu England.
Kwa mujibu wa Kicker, wakali wapya kwenye Ligi Kuu England, Sheffield United wanamtolea macho staa huyo wakimtaka akakipige kwenye kikosi chao. Timu hiyo inataka huduma ya staa huyo mwenye uzoefu mkubwa ili kukifanya kikosi kupambana kukwepa kushuka daraja mapema.
Hata hivyo, Ribery akienda kwenye timu haitakuwa mara ya kwanza kwa mchezaji mwenye jina kubwa kwenye kucheza timu isiyodhaniwa kama vile ilivyotokea kwa Julien Faubert aliyekwenda kujiunga na West Ham akitokea Real Madrid, Carlos Tevez na Javier Mascherano walikwenda kucheza West Ham pia, wakati Paulinho alitoka Guangzhou Evergrande kwenda kucheza Barcelona, Nicklas Bendtner alitoka Arsenal kwenda Juventus, Bebe alitoka Vitoria de Guimaraes akaenda Manchester United, Edgar Davids alienda kuichezea Barnet na Juninho alitoka Atletico Madrid alienda kucheza Middlesbrough.
Sheffield unahusishwa pia na mpango wa kuwanasa wakongwe wengine, beki wa kati Phil Jagielka na kiungo wa zamani wa Chelsea, John Obi Mikel.

Advertisement