Rashford, Aubameyang ni shida mpya England

Tuesday January 14 2020

 

LONDON ENGLAND. KENGELE ya hatari imelia huko Manchester United. Sasa hivi wanahaha namna ya kumtuliza kiungo wao ghali, Paul Pogba abaki Old Trafford. Atabaki vipi?

Bila ya kubeba taji, bila ya kumaliza ligi kwenye Top Four inatajwa kwamba itakuwa ngumu kuendelea kubaki na huduma ya Pogba kwenye kikosi chao hasa ukizingatia kwamba anasakwa na vigogo kama Juventus na Real Madrid ambao siku zote wamekuwa wakitamba kwenye mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, michuano ambayo kila mchezaji wa hadhi ya kiungo huyo wa Ufaransa angependa kucheza. Wakati hilo la Pogba likiwa halijamalizwa, straika Marcos Rashford litakuwa tatizo jipya huko Man United katika kutuliza akili yake ili abaki Old Trafford. Imeelezwa kwamba kama Man United haitafanya kitu cha maana kwenye suala la kubeba mataji hata Rashford naye ataondoka, ukizingatia Real Madrid na Barcelona zote zinahitaji saini yake.

Ndani ya miaka sita na nusu iliyopita, Man United imekuwa haina maajabu.

Jumamosi iliyopita, Rashford alicheza mechi yake ya 200 kwenye kikosi hicho, huku mechi 137 akiwa ameanzishwa. Amefunga mara mbili kwenye mchezo huo kumfanya afikishe mabao 19 msimu huu, 64 akiwa klabuni hapo. Mchanganuo wa mabao yake Rashford amefunga kwa kichwa mara tano, mguu wa kushoto saba na mguu wa kulia mara 52. Kwa namna fulani ametimiza wajibu wake. Je, Man United itafanya nini kumbakiza asishawishike kuondoka kama anavyotaka kufanya Pogba?

Arsenal pia wapo kwenye hatari ya kuwapoteza mastaa wake kama Pierre-Emerick Aubameyang na Alexandre Lacazette, ambapo bila ya shaka watasogelea mlango wa kutokea kama hakutakuwa tena na soka la Ulaya msimu ujao. Wababe hao wa Emirates wamekuwa na rekodi ya kupoteza mastaa wake wengi kwa sababu hiyo, wakiondoka kwenda kusaka mafanikio kwingineko.

Timu nyingine iliyo kwenye hatari ya mastaa wake kuondoka kutokana na kushindwa kubeba mataji ni pamoja na Tottenham Hotspur, ambapo bila shaka straika Harry Kane na Dele Alli hawatakuwa na sababu ya kubaki kwenye timu hiyo miaka miwili ijayo kama hakutakuwa na taji lolote na michuana ya Ulaya.

Advertisement

Advertisement