Ramsey Chelsea, Jorginho Juventus

Turin, Italia. MAURIZIO Sarri bado anataka kuisuka upya Juventus kupitia kwa kiungo fundi wa Kiitaliano, Jorginho na anataka kumtumia kiungo wake Aaron Ramsey kama chambo.

Sarri ndiye alimnunua Jorginho wakati akiinoa Chelsea na sasa anataka kuungana naye kwenye kikosi chake cha Juventus.

Kwa sasa Jorginho ameonekana kuwa mchezaji wa kawaida kwenye kikosi cha Kocha Frank Lampard na Sarri anataka kumrejea Italia ili kuunga naye.

Ramsey aliyejiunga na Juventus msimu uliopita baada ya kuachana na Arsenal, anaweza kurejea Ligi Kuu England kama mpango huo utafanikiwa lakini, safari hii akivaa jezi ya Chelsea.

Ripoti kutoka Italia zinasema kuwa, Chelsea wanaweza kufanya biashara ya wachezaji hao na Sarri wakati huu ambao, Lampard yuko bize kukisuka upya kikosi chake akinasa mastaa wawili wakali, Timo Werner na Hakim Ziyach.

Dili hilo likikamilika basi Sarri ataungana na Jorginho kwa mara ya tatu akicheza chini yake kwani, waliwahi kuwa pamoja katika kikosi cha Napoli kabla ya kumvuta Chelsea na sasa anapambana kumvuta Juventus.