Rabiot apangiwa namba Arsenal

LONDON ENGLAND. UMESIKIA? Kiungo wa Juventus, Adrien Rabiot ameripotiwa kuonyesha dalili zote kwamba, yupo tayari kwenda kujiunga na Arsenal wakati dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi litakapofunguliwa.

Kiungo huyo Mfaransa amekuwa akipata wakati mgumu wa kuanzishwa kwenye kikosi cha Juventus tangu alipojiunga kwa uhamisho wa bure akitokea Paris Saint-Germain mwaka jana. Rabiot hivi karibuni alikanusha taarifa kwamba, ataingia katika mgomo kushinikiza kuihama Juventus, lakini mwenyewe amedai suala la kuachana na timu hiyo halina mjadala.

Arsenal kwa sasa wapo mstari wa mbele kuwania sauni yake, licha ya kuripotiwa watakabiliwa na upinzani mkali kutoka Manchester United na Everton zinazohitaji pia saini yake.

Wakati hilo la kwenda Emirates likipamba moto, Rabiot atakwenda kuvaa jezi namba ngapi atakapotua katika kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta? Rabiot alipotua Juventus alikabidhiwa jezi namba 25, akitumia namba ileile ambayo alivaa akiwa PSG.

Namba hiyo kwa sasa huko Arsenal inapatikana tu baada ya kuachwa wazi na Carl Jenkinson, aliyehama timu hiyo mwaka jana.

Hivyo, Rabiot atakuwa huru kuchukua namba hiyo. Lakini, alipokuwa Parc des Princes, Rabiot aliwahi kuvaa jezi yenye namba ‘7’, ‘6’ na ‘8’ mgongoni. Namba 8 kwa sasa huko Arsenal inavaliwa na Dani Ceballos, ikiwa na maana itakuwa wazi wakati Mhispaniola huyo atakaporejea Real Madrid mwishoni mwa msimu wakati mkopo wake utakapofika mwisho.

Namba 7 na 6 zipo wazi huku Henrikh Mkhitaryan, anayeomba namba 7 kwa sasa yupo kwa mkopo AS Roma, mahali ambako anaweza kubebwa moja kwa moja.

Namba 12 na 13, ambazo zilikuwa zikivaliwa na Stephan Lichtsteiner na David Ospina nazo zitakuwa wazi kwa Rabiot kuchagua kama atataka kuzivaa pale Emirates.