Pochettino sasa anataka kombe Spurs

Muktasari:

Spurs haijashinda ubingwa wowote tangu walipobeba Kombe la Ligi mwaka 2008 na hilo ndilo linalomfanya Pochettino kutaka kufanya kitu kwenye kikosi hicho kuleta mabadiliko.

LONDON, ENGLAND . KOCHA, Mauricio Pochettino amesema kushinda ubingwa ndicho kitu pekee kitakachomfanya ahesabu kuwa amefanikiwa kwenye kikosi cha Tottenham Hotspur.
Kocha huyo ameisaidia Spurs kumaliza ndani ya Top Four kwenye Ligi Kuu England mara nne mfululizo, lakini sasa kitu anachokwama ni kubeba mataji.
Msimu uliopita, Pochettino aliongoza Spurs kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ikiwa ni fainali yake ya pili ya makombe tangu alipotua kwenye kikosi hicho wakati alipotinga fainali ya Kombe la Ligi mwaka 2015.
Spurs haijashinda ubingwa wowote tangu walipobeba Kombe la Ligi mwaka 2008 na hilo ndilo linalomfanya Pochettino kutaka kufanya kitu kwenye kikosi hicho kuleta mabadiliko.
Kwenye dirisha la usajili wa majira ya kiangazi lililofungwa Alhamisi iliyopita, Pochettino ametumia zaidi ya Pauni 100 milioni kuleta majembe mapya kwenye kikosi chake akiwanasa Tanguy N’Dombele, Giovani Lo Celso, Ryan Sessegnon na Jack Clarke kuhakikisha wanatengeneza kikosi matata kabisa cha ubingwa.
Huko nyuma kocha huyo aliwahi kucheza Kombe la FA na Kombe la Ligi si muhimu, lakini sasa wakiwa kwenye uwanja mpya anataka washinda taji lolote ili kunogesha kabati lao la mataji na kuhesabu mafanikio.