Nimeupenda ujeuri wa kocha Zahera

Muktasari:

Ingawa sio vizuri kuuonyesha ujeuri hadharani, kuna wakati mwanadamu analazimika kufanya hivyo ili aweze kutimiza na kufanikisha jambo lake.

KILA mwanadamu ni jeuri. Utofauti ni kiwango cha ujeuri kwa mtu husika na namna ambavyo anaweza kuuficha au kuuonyesha hadharani hasa kwenye kundi la watu.

Ingawa sio vizuri kuuonyesha ujeuri hadharani, kuna wakati mwanadamu analazimika kufanya hivyo ili aweze kutimiza na kufanikisha jambo lake.

Hata hivyo inahitajika ujasiri wa hali ya juu kwa mtu kuweza kuonyesha ujasiri wake hadharani, ni watu wachache ambao wamekuwa na uwezo wa kufanya hivyo pasipo kujali nini kitamtokea.

Moja kati ya watu ambao kwao hawana hofu ya kuonyesha ujeuri wao mbele ya hadhara, unaweza kumpata binadamu kama Mwinyi Zahera, kocha mkuu wa Yanga anayetokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Ndani ya muda mfupi alioitumikia timu hiyo tayari amefanikiwa kuonyesha ujeuri wa kusimamia misimamo yake na kuishi kinyume na utamaduni wa muda mrefu ambao ulikuwa umezoeleka sio tu ndani ya Yanga bali soka la Tanzania kiujumla.

Katika kushughulikia utovu wa nidhamu wa wachezaji wake, Zahera ameanzisha utaratibu wa kuwakata mshahara wachezaji wanaoshindwa kutii vigezo, masharti na vipengele ambavyo vipo kwenye mikataba yao ya kuitumikia klabu hiyo tofauti na ilivyokuwa hapo kabla.

Hii inamaanisha kwamba mchezaji atalazimika kuwa makini katika kutii maagizo na maelekezo ambayo atapatiwa ndani ya timu kwa hofu ya mshahara wake kukatwa.

Lakini pia ni huyu Zahera ambaye ameanzisha utaratibu wa kuhakikisha mchezaji wa Yanga anapata nafasi ya kupangwa kwenye mechi kulingana na ushiriki na ufanisi wake katika programu za mazoezi ya timu hiyo na sio vinginevyo.

Amezika ule utamaduni wa mchezaji kupangwa kutokana na jina au jinsi anavyopendwa na mashabiki wa timu hiyo ambao ulidumu kwa muda mrefu ndani ya Yanga jambo ambalo lilikuwa likichangia uwepo wa matabaka kwenye timu.

Tayari tumeshuhudia akina Thaban Kamusoko, Amissi Tambwe, Beno Kakolanya wakihukumiwa na utamaduni huu mpya ambao Zahera ameuanzisha wa mchezaji kupatiwa nafasi kutokana na ufanisi wake kwenye programu za timu kuelekea kwenye mchezo husika.

Pia tumeona na kusikia Zahera akitangaza hadharani kuwatimua na kuwasimamisha wachezaji wa timu hiyo wanapochelewa kambini, mazoezini au kushindwa kufuata maelekezo ambayo wamekuwa wakipatiwa na benchi la ufundi.

Utamaduni ambao umeonekana kuwakera baadhi ya mashabiki na wanachama wa Yanga wakiamini kwamba unaweza kuathiri ufanisi wa wachezaji wao lakini kwa jicho la tatu una faida kubwa kwa timu, wachezaji binafasi na soka la Tanzania.

Kwa muda mrefu suala la utovu wa nidhamu kwa wachezaji wa Kitanzania limekuwa tatizo sugu ambalo huchangia kuporomosha viwango vyao na kufanya vibaya kwa kwa timu zetu kwenye mashindano mbalimbali ambayo zimekuwa zikishiriki hasa ya kimataifa.

Utovu wa nidhamu umekuwa ni sumu ambayo hutengeneza mpasuko ndani ya timu unaotokana na matabaka yanayoibuka baina ya wachezaji ambao baadhi hujiona ni wakubwa kuliko klabu na wale ambao wanaonekana kama wa daraja la chini.

Tabia hizi za utovu wa nidhamu zimekuwa zikifahamika lakini hufichwa kwa hisia kwamba zitavuruga timu na kufanya zipate matokeo mabaya.

Hata hivyo Zahera amefanikiwa kuvunja utamaduni huo wa kuficha maovu na kuwachukulia hatua watovu wa nidhamu na badala yake ameanza taratibu kujenga msingi wa kufanya mambo kwa weledi kwa wachezaji wetu.

Inawezekana Zahera akaonekana mbaya lakini tufahamu kuwa anavyofanya hivyo, anaongeza umakini kwa wachezaji kujali na kuthamini muda kwenye kazi yao na kutambua wajibu na majukumu wanapokuwa nje na ndani ya uwanja lakini pia kuheshimu mikataba yao.

Zahera ni kama panya aliyeamua kujitoa muhanga kumfunga paka kengele baada ya kundi kubwa la makocha na viongozi wa timu mbalimbali hapa nchini kushinda kunyoosha nidhamu na kujenga msingi wa weledi kwa wachezaji wetu.

Tulihitaji makocha na viongozi wa soka wenye ujeuri kama wa Zahera ili watusaidie kuvunja utamaduni mbovu wa kutotambua wajibu na majukumu kwa wachezaji lakini kwa bahati mbaya hatukuweza kuwapata na huu ndio muda mwafaka kwao kujifunza.