Msuva njiapanda Morocco

Monday June 15 2020
msuva pic

MATUMAINI ya nyota wa Difaa El Jadida, Simon Msuva kuwa Ligi Kuu Morocco itarejea hivi karibuni, yameanza kufifia kutokana na Serikali ya nchi hiyo kuongeza siku za kukaa ndani kama sehemu ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa covid-19.

Serikali ya Morocco imeripotiwa kuongeza siku za watu kukaa ndani hadi Agosti 8, uamuzi ambao umemfanya Msuva kuona pengine Ligi hiyo maarufu kama Batola Pro inaweza kutorejea tena.

“Nilitamani tuendelea na Ligi hivi karibuni ila haiwezekani kwa sababu ya hali ilivyo, ni ngumu kwa sasa kuendelea na Ligi maana maambukizi ni makubwa,” alisema.

Upande wake Nickson Kibabage, alisema kinachofanyika Morocco ni mapambano hivyo pamoja na kuwa amemisi kucheza soka, atakuwa sehemu ya mapambano hayo.

“Nitaendelea kukaa ndani hadi hapo mambo yatakuwa shwari, nimemisi kucheza soka lakini hakuna jinsi,” alisema beki huyo.

Ripoti zimedai serikali iliongeza hali ya dharura hadi Agosti 8 ‘marufuku’, kwa kuzingatia rasimu ya sheria kutoka kwa Katibu Mkuu wa Serikali, ambaye alitaka nyongeza ya miezi mbili.

Advertisement

Serikali ilitangaza habari hiyo baada ya mkutano, siku moja tu kabla ya marufuku ya mwanzo ya wananchi kuzurula hovyo kufikia ukomo siku chache zilizopita.

Mamlaka ya Morocco ilifanya uamuzi huo baada ya kugundua kuwa, maambukizi ya virusi vya corona nchini kwao hayakupungua, wakilinganisha na mataifa mengine.

Morocco sasa imethibitisha kesi 8,438 za virusi vya corona.

Advertisement