Mpepo awazia Ligi ya Mabingwa Afrika

STRAIKA wa Buildcon ya Zambia, Eliuter Mpepo ameitolea macho nafasi ya msimu ujao kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na chama lake ambalo Jumamosi liliibuka na ushindi mwembamba mbele ya Forest Rangers.

Wakiwa ugenini Buildcon ya Mpepo waliitandika Forest Rangers bao 1-0 huku chama la Mtanzania mwingine, Hassan Kessy likitoka sare ya bao 1-1 na Nkwazi.

Mpepo alisema wapo nafasi ya pili kwenye Ligi ya ukanda wao hivyo wanatakiwa kufanya vizuri kwenye michezo miwili iliyosalia ili wamalize vinara wa kundi B .

“Karibu kila mechi nimekuwa nikicheza, tumepishana pointi tatu na Green Eagles ambao wanaongoza, wao wanapointi 32, sisi ni 29. Kabla ya mechi ambayo tulishinda Jumamosi, wiki iliyopita nyuma tulicheza na wakiwa Kessy na tulitoka sare 1-1,” alisema Mpepo

Mshambuliaji huyo alifafanua kwa kusema, “Iko hivi Ligi ya huku inachezwa kwa kanda mbili, kila kanda inatimu 10, watakaoongoza kwenye kila kanda wanafuzu Ligi ya Mabingwa, nafasi za pili ni Kombe la Shirikisho.

“Msimu ukimalizika wale walioongoza kwenye kanda hizo, wanakutana kutafuta bingwa wa msimu huku wale walioshika nafasi ya pili nao watacheza mchezo kutafuta bingwa wa kombe la Barclays.”

CHAMA LA KESSY HALI TETE

Mambo sio mambo kwa chama la Kessy ambalo na lenyewe lipo ukanda B kwenye Ligi ya Zambia, Nkana wapo wanafasi ya saba huku wakiwa nyuma kwa michezo miwili, wanahitajika kufanya kazi ya zaida ili kumaliza kwenye nafasi za juu.