Morrison anapotuonyesha sura yake halisi

Thursday June 25 2020
Morrison pic

Yanga wanapasua vichwa na jambo moja tu sasa juu ya majaliwa ya mshambuliaji wao Bernard Morrison ambaye anarusha ngumi kisha klabu yake ikijibu hatua ambayo inawachanganya mashabiki wake wakitafuta nani ameanza kumrushia ngumi mwenzie.

Morrison anadai hana mkataba zaidi na Yanga ukiondoa ule wa miezi sita ambao aliusaini awali wakati anatua nchini kwa mara ya kwanza katika usajili wa dirisha dogo lakini klabu yake nayo inasisitiza wanachofahamu wao mkataba wa mshambuliaji huyo utamalizika Julai mwaka 2022 baada ya pande hizo mbili kukubaliana kuongeza mkataba mwingine na alishausaini.

Hatua hii imezua utata mkubwa huku mashabiki na wanachama wa klabu hiyo wakishindwa kutambua waamini kipi kati ya kauli hizo mbili -- ile ya mchezaji wao ambaye anadai hana mkataba wa kuongeza au ile ya uongozi wao wanaosema mchezaji huyo ni mali yao.

Mashabiki wanachanganyikiwa zaidi wanaposikia kuna hatua ya mchezaji wao huyo kuhamia upande wa pili na wakikumbuka kazi ambayo Morrison ameifanya katika miezi sita tu vichwa vinawauma zaidi.

Ukisikiliza kauli ambayo Morrison anaitoa katika madai yake unapata shaka zaidi lakini kama ukiamua kujiongeza unaweza kumuelewa zaidi mshambuliaji huyo kwanini Yanga walimkuta kama mchezaji huru.

Hatua ya kwanza ambayo Morrison anatupa wasiwasi ni pale anaposema aliichezea timu hiyo mechi mbili za awali katika ligi akiwa hana mkataba, ukisikia kauli hii kisha ukaoanisha na taratibu zinazopaswa kufanyika hadi mchezaji apewe leseni ya kucheza Ligi Kuu utagundua kwamba kuna kitu kinapungua katika stori za Morrison.

Advertisement

Morrison anatakiwa kujipanga vyema kabla ya kuja mbele ya vyombo vya habari kisha kuzungumza kwani mchezaji hawezi kucheza ligi bila ya kuwa na leseni ambayo nayo huwezi kuipata kama hautakuwa na mkataba.

Inawezekana kuna utulivu ambao unapungua kwake kabla ya kuja kuzungumza na hili linaweza kumfanya kila wakati kuwa na matatizo ya kimkataba sio tu Yanga bali sehemu mbalimbali ambazo atakuwa akienda.

Mkataba ambao Morrison aliusaini wa miezi sita ndio uliotumika kumpatia leseni mpaka akaanza kuitumikia Yanga katika mchezo wa kwanza dhidi ya Singida United kule Singida na sio Azam FC ambao aliushuhudia akiwa jukwaani pale Uwanja wa Taifa tena akikaa katika jukwaa letu waandishi wa habari.

Nilimsikia awali katika kesi ya namna hii ya mkataba wake na Yanga akijichanganya kwamba Simba walikuwa wakimtaka na kuna wakala alitumwa na Rais wa Klabu kuja kumshawishi ajiunge na Wekundu wa Msimbazi, lakini madai hayo yalikanushwa kirahisi na Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa akimtaka mchezaji huyo kuwa makini na kauli zake kwa kuwa Simba haina Rais badala yake ina Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi na Mtendaji Mkuu.

Hii inatosha kupata picha kwamba Morrison ana shida ya uelewa kama sio kujipanga zaidi katika kuongea kwake kwani kauli zake zimekuwa zikijichanganya na kuleta utata katika unyoofu wake. Hii inaweza kumshushia heshima katika uchezaji wake wa soka.

Kesi hizi hapa nchini tulishazisahau muda mrefu na zinashtua kuonekana zinarudishwa na mchezaji kama Morrison ambaye ameshacheza ligi kubwa na klabu kubwa Afrika kama Orlando Pirates ya Afrika Kusini ambayo imepiga hatua kubwa kimaendeleo kuliko Yanga.

Wapo wachezaji ambao walitakiwa kujifunza mambo mbalimbali kutoka kwa Morrison lakini sicho ambacho mchezaji husika anajaribu kukionyesha sasa na inawezekana kikawa chanzo cha kuwarudisha wachezaji wengi nyuma.

Nina wasiwasi Morrison kama ataendelea kucheza kwa muda mrefu kisha asijirekebishe na utulivu wa akili yake kuna uwezekano mkubwa siku moja ataturudisha katika enzi za migogoro ya mchezaji kusaini klabu mbili tofauti kama ambavyo tuliyashuhudia matukio hayo huko miaka ya nyuma.

Advertisement