Mo Rashid :KMC imenipa faraja

Thursday December 13 2018

 

By OLIPA ASSA

STRAIKA Mohamed Rashid 'Mo Rashid' ameizungumzia timu Simba iliyompeleka kwa mkopo KMC kwamba  itatisha kwenye  michuano ya ligi ya Mabingwa Afrika, akidai ina wachezaji wazoefu na wanaoweza kuamua mchezo.
Simba imewafuata Nkana ya Zambia watakayocheza nayo Jumamosi ya wiki hii, baada ya kuibuka na ushindi mnono wa jumla mabao 8-1 dhidi ya Mbabane Swallows, wakishinda manne Uwanja wa Taifa na manne ugenini.
Ameliambia Mwanaspoti kwamba Simba, imekamilika kila idara na kukiri kwamba ndio sababu ya yeye kutolewa kwa mkopo baada ya kushindwa kupata namba mbele ya wakongwe Emmanuel Okwi na Meddie Kagere.
"Simba ina nafasi kubwa kutinga hatua ya makundi kwenye michuano ya ligi ya Mabingwa, kwanza kuna ushindani wa namba kwa wachezaji wenyewe kwa wenyewe pia ina ushindani dhidi ya wapinzani wao, binafsi nawatakia kila raheli,"anasema.
Mo Rashid ametambulishwa rasmi leo katika timu yake mpya ya KMC, amezungumzia maisha atakayoanza kuishi ndani ya klabu hiyo kama yatampa mwelekeo wa nini atafanya msimu huu.
"Kabla ya kutambulishwa nilikaa kikaa na kocha wa timu hii mpya, nimegundua alikuwa ananifuatilia tangu nipo Prisons, kaniambia nini anachokitaka kwangu, nina furaha kuwepo hapa.
"Hata nilipokuwa naondoka Simba nilikaa kitako na kocha wa Simba, Patrick Aussems naye alinishauri mengi na kuniambia nina kitu cha tofauti isipokuwa nipate timu nitakayoanza katika kikosi cha kwanza,"anasema.

Advertisement