Mbappe apiga manne ndani ya dakika 13

Muktasari:

  • Mshambuliaji kinda wa Ufaransa, Kylian Mbappe,19, amethibitisha kuwa hakubahatisha alipong’ara katika fainali za Kombe la Dunia 2018 huko Russia, baada ya jana kutumia dakika tisa kuifungia mabao matatu ‘hat trick’ akiifunmgia PSG mabao manne, katika mchezo wa Ligue 1 wakiifunga Lyon mabao 5-0.

Paris, Ufaransa. Mshambuliaji kinda wa Ufaransa, Kylian Mbappe,19, ameendelea kuonyesha kiwango bora na kuthibitisha kuwa atakuwa tishio siku zijazo.

Mbappe juzi alitumia dakika tisa kufunga mabao matatu ‘hat trick’ na dakika 13 kufunga mabao manne katika ushindi wa mabao 5-0 ilioupata Paris St Germain dhidi ya Lyon katika mchezo wa Ligi Kuu Ufaransa ‘Ligue 1’.

Ushindi huo uliiwezesha PSG, iliyo kileleni kuzidi kupanua pengo la pointi kufikia nane, kila timu ikiwa imecheza mechi tisa.

Nahodha wa Brazil, Neymar, ndiye aliyeanza kujipatia mabao kwa mkwaju wa penalti dakika ya tisa kabla ya PSG kupata pigo baada ya mchezaji wake Presnel Kimpembe kulimwa kadi nyekundu dakika ya 32.

Mbappe alianza kuonyesha uwezo wake kwa kufunga bao la pili la mchezo huo katika dakika ya 61 kabla ya kuongeza mengi dakika za 66, 69 na 74.

Mshambuliaji huyo alianza kuchomoza katika medani ya soka baada ya kung’ara katika fainali za 32 za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini Russia, alipochangia kuipa Ufaransa ubingwa akifunga mabao manne na kuchaguliwa kuwa chipukizi bora wa fainali hizo.