Mastaa hawa huwaambii kitu kwa Cristiano Ronaldo

TURIN, ITALIA. HAKUNA ubishi, Cristiano Ronaldo ni mmoja wanasoka bora kabisa wa muda wote.

Fowadi huyo gwiji wa Ureno ameshinda tuzo ya Ballon d’Or mara tano, akifunga mabao kibao na kubeba mataji mengi tu kwenye klabu alizocheza England, Hispania na Italia.

Ronaldo aliisaidia pia Ureno kubeba ubingwa wa Euro 2016.

Staa huyo, ambaye alitimiza umri wa miaka 36, Februari mwaka huu, amehamasisha vijana wengi sana kupenda soka na kuamua kucheza, akiwamo supastaa wa Paris Saint-Germain na Ufaransa, Kylian Mbappe.

Katika mechi moja ya UEFA Nations League iliyopigwa hivi karibuni kati ya Ufaransa na Ureno, Ronaldo na Mbappe walionekana wakifuhia jambo pamoja wakati wa mapumziko.

Baada ya mechi, Mbappe alituma ujumbe wake wa Twitter na kuandika neno “shujaa” sambamba na picha ya taji na emoji ya mbuzi ikiwa ni ujumbe kwa shujaa wake huyo.

Hata hivyo, Mbappe si staa pekee kwenye kizazi hiki cha soka kwa sasa ambaye hadharani amekiri ni shabiki mkubwa wa Ronaldo na yupo kwenye soka kwa ajili ya mkali huyo wa kimataifa wa Ureno.

Hawa hapa mastaa wanaotamba kwa sasa kwenye soka ambao huwaambii kitu kuhusu Ronaldo. Ni shujaa wao.

Erling Haaland

Straika staa wa Borussia Dortmund, Erling Haaland ni moja ya makinda hatari sana kwenye soka kwa sasa, lakini mkali huyo wa Norway aliwahi kusema pengine asingekuwa mwanasoka kama asingekuwapo Ronaldo.

Hayo ni maneno yake mwenyewe mshambuliaji huyo anayefunga mabao tu kama anavyojisikia.

“Ningependa sana kukutana naye na kumwambia asante kwa sasa nimekuwa mwanasoka kwa ajili yake,” alisema straika huyo kinda mapema mwaka huu.

“Kwangu mimi, siku zote atabaki kuwa shujaa wangu.”

Marcus Rashford

Wala haihitaji nguvu sana, tazama tu friikiki za Marcus Rashford anavyopiga, unaona kabisa anajaribu kuiga mbinu za Ronaldo. Kilichopo ni kwamba Rashford wakati anakua amekuwa akimtazama sana Ronaldo na soka lake.

Mwaka 2018, Ronaldo alimtumia Rashford jezi yake ya Real Madrid iliyokuwa imesainiwa na kuandika maneno haya “To Marcus. Keep up the good work”. Maneno ambayo yalikuwa yameandikwa upande wa mgongoni wa jezi hiyo.

Matthijs de Ligt

Matthijs de Ligt alikuwa akijaribu kujifananisha yeye ni Ronaldo kipindi alipokuwa mdogo akicheza soka na wenzake kwenye bustani zao. Mwaka 2019, beki huyo Mdachi alifanikiwa kuwa kwenye timu moja na Ronaldo aliposajiliwa na Juventus kutoka Ajax.

“Niseme tu siku zote nilitaka kuwa Cristiano Ronaldo kipindi hicho nilipokuwa nacheza soka kwenye bustani za nyumbani kwetu,” alisema De Ligt alipozungumza na jarida la Uholanzi la VI.

“Hasa nyakati hizo ni zile alizokuwa akiichezea Manchester United. Jezi yangu ya kwanza ya soka ilikuwa ya Ronaldo kwa kipindi kile.”

Joao Felix

“Cristiano shujaa wangu tangu nikiwa mdogo, ni mfano wa kila kitu kwangu,” alisema Felix alipozungumza na Record mwaka 2019. Staa huyo wa Atletico Madrid aliongeza “Nilikuwa bado mdogo wakati alipokuwa mwanasoka bora duniani. Ni wa kipekee. Anafanya soka kuwa historia. Nilifurahi sana aliponisifia.”

“Watu siku zote wamekuwa wakiniuliza kama naweza kufikia viwango vya Cristiano na siku zote nimekuwa nikiwaambia kitu kile kile, Cristiano ni wa kipekee na hana mbadala. Kitu ambacho nataka ni kuwa Joao Felix.”

James Maddison

Kiungo wa Leicester City, James Maddison alikuwa akiishabikia Manchester United kipindi anakua na amekuwa akimpa sifa kubwa Ronaldo akiamini ni bora kuliko Lionel Messi hadi sasa.

“Shujaa wangu ni Cristiano Ronaldo; siku zote nimekuwa nikimtazama wakati nakua na ukizingatia nilikuwa shabiki wa Man United. Kumbukumbu yangu ni ile mechi ya ushindi dhidi ya Bayern Munich na baba yangu alishangilia na mimi kwa kukimbia kuzunguka meza,” alisema kiungo huyo mshambuliaji alipozungumza na Coventry Telegraph mwaka 2015.

Harry Kane

Straika, Harry Kane unaweza kumwona ni mzoefu kwenye soka la kulipwa kutokana na kile anachokifanya ndani ya uwanja akiwa na Tottenham Hotspur na England, lakini Mwingereza huyo amezidiwa miaka minane na Ronaldo, hivyo alikuwa akimtazama fowadi huyo wa Ureno wakati anakua.

“Nilimwomba jezi yake,” alisema Kane baada ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Real Madrid na Tottenham mwaka 2017.

“Ni shujaa wangu mkubwa sana, nilikuwa namtazama wakati nakua. Ilikuwa jezi bora kabisa kuwa nayo na nimeweka kwenye fremu. Nilimpa jezi yangu, sijui atakuwa ameifanyia nini.”

Vinicius Jr

Ronaldo alionekana uwanjani Bernabeu, Machi 2020 wakati Vinicius Jr alipoifungia bao Real Madrid kwenye mchezo dhidi ya Barcelona na kisha akashangilia kwa staili ya Mreno huyo inayofahamika kwa jina la ‘Siiiiu!’. Baada ya mechi hiyo, kinda huyo wa Kibrazili, Vinicius alithibitisha kupitia ukurasa wake wa Instagram, Ronaldo ni shujaa wake kwenye mchezo wa soka na kitu ambacho amekuwa akikifanya uwanjani ni kuiga mambo ya supastaa huyo wa Juventus.

Mason Mount

Staa wa Chelsea, Mason Mount, kama ilivyokuwa kwa makinda wengine matata kwenye mchezo wa soka, alitumia saa nyingi sana za utotoni kwake kujaribu kuiga mapigo ya friikiki za Ronaldo.

Jambo hilo lilionyesha dhahiri jinsi Mwingereza huyo anavyojaribu kumfuatilia Ronaldo na kuonyesha kwamba yeye ni shabiki mkubwa wa mchezaji huyo.

Kwenye video zilizowekwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, Mount ameonyesha kuwa mahiri zaidi kwenye kupiga friikiki za mtindo wa Ronaldo kuliko kinda mwingine yeyote kwenye umri wake.

Gabriel Martinelli

Kinda wa Arsenal, Gabriel Martinelli ni mchezaji mwingine ambaye kwenye makuzi yake amekuwa akimhusudu sana Ronaldo. Martinelli angeweza kumtaja Ronaldo wa Brazil kuwa ni shujaa wake, lakini humwambii kitu kwa Mreno.

“Shujaa wangu ni Cristiano Ronaldo,” alisema Mbrazili huyo alipozungumza na Goal mwaka 2020. “Namhusudu sana kwa uwezo aliokuwa nao, anavyopambana na kila kitu ...kwa mambo yake binafsi ni tuzo anazobeba.

“Ni mtu asiyetosheka, siku zote anahitaji zaidi na zaidi. Hicho ndicho kitu hata mimi ninachokitaka, siku zote kuwa mtawala. Yeye ni mfano mzuri wa jambo hilo.”

Raheem Sterling

Wakati alipokuwa akikipiga Liverpool, Raheem Sterling alikiri gwiji la Man United, Ronaldo alikuwa mmoja wa mashujaa wake kwenye mchezo wa soka. Kwa sasa winga huyo Mwingereza anakipiga kwenye kikosi cha Manchester City na hajaacha kuzungumzia mambo mazuri ya kuhusu Ronaldo licha ya kuwa kwenye viwango vya kuchuana naye.

“Nilikuwa nikimwangalia Cristiano Ronaldo,” alisema Sterling alipozungumza na The Mirror mwaka 2014,

“Ni mtu ambaye siku zote amekuwa shujaa wangu...lakini sisemi hakukuwa na wachezaji wengine niliokuwa nikiwatazamana hakuna ubishi kila mtu anataka kuwa bora duniani.”

Bruno Fernandes

Mashabiki wa Manchester United wana supastaa mwingine wa Kireno wanayemkubali sana Old Trafford kwa sasa, Bruno Fernandes.

Lakini, kiungo huyo fundi wa mpira, Fernandes alifichua Februari mwaka huu Ronaldo alikuwa sababu kubwa ya yeye kwenda kujiunga na Man United.

“Mimi ni shabiki wa Cristiano Ronaldo na ndiye mchezaji ninayemfuatilia zaidi,” alisema Fernandes alipozungumza na Sky Sports.

“Wakati Cristiano alipoibukia Manchester, alikuta mambo mengi mazuri sana mwanzoni mwa maisha yake ya soka na hakika alifurahia mafanikio makubwa. Ndio ilikuwa ndoto yangu pia kwenda kuichezea Manchester United.”

Justin Kluivert

Baba yake Justin Kluivert, Patrick, alikuwa mchezaji mkubwa sana, lakini staa huyo wa kimataifa wa Uholanzi ni shabiki mkubwa wa Ronaldo.

Wakati ukifikiria Justin angedai baba yake ni shujaa wake, lakini mkali huyo wa zamani wa Ajax humwambii kitu kuhusu Ronaldo.

“Kwa kile anachofanya ndani na nje ya uwanja, shujaa wangu ni Cristiano Ronaldo,” alisema Justin akiiambia DAZN, per Goal.

“Nimekuwa nikimhusudu sana tangu nilipokuwa mtoto na bado namfuatilia, lakini shida ni kwamba sina picha yoyote niliyowahi kupiga naye.”

Memphis Depay

Baada ya kusajiliwa na Manchester United, Mei 2015, Memphis Depay alifichua Ronaldo ndiye mtu anayemhamasisha zaidi kwenye mchezo wa soka. Alipotua Old Trafford, Depay alitaka jezi Namba 7 iliyowahi kuvaliwa na Ronaldo alipokuwa kwenye kikosi hicho cha miamba ya Man United.

“Ni heshima kubwa sana kuwa na jina kubwa kama lake, lakini kwa kusema ukweli, namkubali sana,” alisema Depay alipozungumza na BBC Sport.

“Ni shujaa wangu na ni mchezaji mkubwa sana, pengine mkubwa zaidi duniani. Namtazama sana. Natazama friikiki zake na mikimbio yake uwanjani.”

Bukayo Saka

Kinda wa Arsenal, Bukayo Saka naye ni mwanasoka mwenye uchu mkubwa wa kufika mbali kwenye mchezo huo, lakini jambo kubwa analofanya ni kujaribu kuiga kile ambacho Ronaldo amekuwa akikifanya.

“Cristiano Ronaldo,” alisema Saka, alipozungumza na Per Goal alipoulizwa ni mwanasoka gani ambaye ni shujaa wake. “Napenda msimamo wake. Siku zote anataka kuwa bora, anapambana ndani na nje ya uwanja akiufanya mwili wake kuwa bora. Ni mchezaji tofauti sana. Siku zote amekuwa akielekeza akili yake kwenye mchezo,anapambana na ninachofanya ni kujaribu kuwa bora kama yeye.”