Masoud aula saini mwaka mmoja kuinoa AS Kigali

Muktasari:

  • Kocha msaidizi wa zamani wa Simba, Mrundi Masoud Djuma amesaini mkataba wa mwaka mmoja wa kuifundisha AS Kigali inayoshiriki Ligi Kuu Rwanda.

Dar es Salaam. Ukisema cha nini mwenzio anasema atakipata lini? Ndicho kilichotokea kwa Kocha Masoud Djuma baada ya kutupiwa virago na Simba leo Ijumaa ameenda uwanjani kushuhudia kikosi chake kipya cha AS Kigali kinacheza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Rwanda dhidi ya Musanze Fc.
Djuma aliyekuwa kocha msaidizi wa Simba, amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuifundisha timu hiyo akiwa kocha mkuu.
Djuma aliachana na Simba baada ya kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba wake uliobaki mwaka mmoja kwa kile kilichoelezwa ni kutokuwa na uhusiano mzuri na bosi wake Patrick Aussems.
Djuma amesema anaamini kila jambo hutokea likiwa na maana kubwa na ndiyo maana haijachukuwa muda mrefu kwake kupata timu ya kuifundisha.
"Nipo uwanjani nawaangalia wachezaji wangu, naifahamu hii timu na ina wachezaji wazuri, mapungufu madogo madogo yatarekebishika kwani kila timu inakuwa na changamoto upande wa ufundi.
"Nimeamua kusaini mkataba wa mwaka mmoja na AS Kigali baada ya kufikia makubaliano yetu na kuridhika na kile nilichokihitaji, nilikuwa na ofa nyingine nje ya timu hii ila kuna vitu vimenifanya nisaini mkataba huu," alisema Djuma.