Mambo matatu kuibeba Yanga SC

Dar es Salaam. Klabu ya soka ya Yanga, mbali ya kufaidika na mfumo mpya wa uendeshaji, pia itapata fursa ya mafunzo kwa wachezaji, makocha na viongozi kutoka klabu ya Sevilla ya Hispania.

Hayo yamo katika mkataba uliosainiwa juzi usiku kati ya Yanga na kampuni inayoendesha Ligi Kuu ya Hispania, La Liga chini ya udhamini wa Kampuni ya GSM ambayo katika hatua ya mwanzo itatoa Euro 80,000 (zaidi ya Sh205 milioni) kulipia gharama za uendeshaji kwa awamu ya kwanza yenye miezi mitano.

Mkataba huo ambao msingi wake ni kuifanya Yanga kuwa na mfumo wa kisasa wa uendeshaji, umeenda mbali zaidi ambapo licha ya kucheza mechi mbili kwa mwaka baina ya Sevilla na Yanga, pia utatoa fursa kwa wachezaji chipukizi kujiunga na shule ya michezo ya timu hiyo yenye historia kubwa ya soka.

Kwa mujibu wa ofisa habari wa Yanga, Hassan Bumbuli kutakuwa na mechi mbili kwa mwaka baina ya timu yao na Sevilla ambayo moja itafanyika Hispania na nyingine hapa nchini.

“Mbali ya mechi, Yanga itakuwa inafanya ziara za kimafunzo nchini Hispania kwa mwaliko wa na hakuna timu nyingine ambayo itawakaribisha zaidi ya Sevilla. Hata wao wakija hapa nchini, sisi tutakuwa wenyeji wao na kutoa fursa ya kuutangaza utalii wa nchi,” alisema Bumbuli.

Aliongeza kuwa klabu ya Sevilla kupitia La Liga pia itakuwa inatoa mafunzo ya makocha na viongozi hasa wa masuala ya soka kwa klabu yao.

“Tofauti na watu wanavyofikiria, mkataba umeenda mbali zaidi ambapo hata wachezaji wetu chipukizi watapata nafasi ya kujiunga na timu ya Akademi ya Sevilla. Watakapoata timu za kujiunga nazo, Sevilla, Yanga, La Liga chini ya udhamini wa GSM watakamilisha ‘dili’ hilo na klabu yetu kufaidika.”

Alifafanua kuwa wataalamu wa Sevilla na La Liga pia watakuwa wanakuja nchini kufanya mafunzo mbalimbali ya uongozi kwani mfumo ambao Yanga itakuwa inautumia lazima uendane na ujuzi na uzoefu mpya katika masuala ya uongozi.

Mkataba wenyewe

Mkataba wa Yanga, La Liga na GSM ni wa miaka mitatu ambao utakuwa na awamu nne. Awamu ya kwanza itakuwa si chini ya miezi mitano itagharimiwa na kampuni ya GSM.

GSM itagharimia shughuli mbalimbali za wataalamu wa La Liga ambao wakuwa na ofisi kwenye jengo la kampuni hiyo lililopo Barabara ya Samora jijini Dar es Salaam.

Katika kipindi hicho, La Liga itatoa mapendekezo mbalimbali kwa kamati ya mabadiliko ya Yanga chini ya mwenyekiti Alex Mgongolwa na kujadiliwa na kamati ya utendaji ya Yanga na wadau wengine.

Mbali ya mapendekezo ya mfumo wa uendeshaji, pia kutakuwa na suala mabadiliko ya Katiba ya klabu ambapo mpango wa klabu ya Yanga ni kuwahsirikisha wanachama na wadau wote kwa muda wa siku 21.

Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla alisema wawakilishi wa matawi kutoka kila pande za Tanzania watapata mafunzo maalumu jijini Dar es Salaam na kupewa makabrasha ambayo watayatumia kuendesha elimu ya mabadiliko hayo pindi watakaporejea kwenye matawi yao.

“Gharama hizi za awali, zitakuwa chini ya GSM ambayo imejitolea na hatutalazimika kumlipa chochote. GSM kama mdhamini, imekuwa mstari wa mbele kuona klabu yetu inafanikiwa katika kila idara,” alisema Dk Msolla.

Hersi Said, ambaye ni mkurugenzi wa uwekezaji GSM alisema watasaidia mchakato huo ili Yanga ijitegemee na kuondokana na hali iliyo nayo sasa.

“Huwezi kuingia mkataba na kuwekeza kwenye kampuni ambayo unajua haitaweza kukufikisha pale ambapo unataka kufika.

Mgongolwa alisema hatua waliyofikia inaleta matumaini ya mafanikio katika mchakato huo, “tumekuwa tukipokea simu zaidi ya 300 kwa siku, wote hao wamekuwa wakitoa maoni kuhusiana na mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji, tumewasilikiza na tunasubiri kupata mapendekezo ya La Liga na kufanya majumuisho ya pamoja na kamati ya utendaji wa Yanga kabla ya kutoa taarifa rasmi kuwa mfupo upi unafaa.”

Naye mkurugenzi wa Biashara wa Kimataifa wa La Liga, Juan Botella alisema wamefurahi kuingia mkataba na Yanga ambayo inakuwa ya kwanza katika Ukanda wa Afrika kufanya hivyo.

Botella alisema kuwa kampuni yao ina wataalam wa kimataifa ambao watashirikiana na klabu ya Sevilla ili kuhakikisha Yanga inakuwa na mfumo wa kisasa wa uendeshaji na kupata mafanikio.

Naye mkurugenzi wa Kimataifa wa Masoko na Biashara wa Sevilla, Oscar Mayo alisema makubaliano yao na Yanga yanalenga kuleta maendeleo katika nyanja za ufundi, masoko na uongozi, huku rais wa klabu hiyo Jose Castro Carmona akisema anaamini Yanga itafanikiwa na kuwa ya mfano Tanzania na Afrika.

JK atia neno

Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alipongeza hatua ya Yanga kuelekea kwenye mabadiliko huku akikumbushia majaribio mengine mawili yaliyoshindikana kwenye mabadiliko.

Kikwete alisema Yanga ilianza mabadiliko enzi za uongozi wa katibu kkuu, George Mpondela (marehemu) na baadaye chini ya

uongozi wa uenyekiti wa Yusuf Manji.

Alisema kuwa mchakato wa sasa unaonyesha mwanga wa Yanga kufikia katika hatua ya mabadiliko ambayo anaamini yataleta tija.

“Yanga ilishindwa kufikia hatua hiyo kutokana na kukosa elimu kwa wanachama kujua nini wanataka kufanya wakati huo, na kushindwa kufikia hatua za mwisho, naamini safari hii itakuwa tofauti na Yanga itafikia lengo lilowekwa,” alisema Kikwete.