MAGORI: Kashfa ya upilizaji dawa ilitutesa CAF

KATIKA mfululizo wa makala za aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Simba na Mshauri Mkuu wa sasa wa Bilionea wa klabu hiyo, Mohammed Dewji, Crescentius Magori, jana Jumapili tuliona alivyofunguka kuhusu usajili unavofanywa na jinsi Simba ilivyo na kikosi kipana.

Magori pia alisema upana wa kikosi hicho cha Msimbazi na namna kilivyobeba nyota mbalimbali baadhi ya wachezaji waliokuwa wakionekana mastaa kama Clatous Chama ama Ibrahim Ajibu ni lazima wakomae la sivyo itakula kwao.

Leo Jumatatu tunaendelea naye akiwa ndio anaelekea mwishoni mwa mahojiano yake maalumu na Mwanaspoti, akikichambua kikosi cha Yanga na kufichua ishu nzima ya tuhuma za kuhusika kupuliza dawa zenye kemikali hatarishi ili kuwadhoofisha wapinzani wao kwenye mechi za CAF?

Kuna ukweli wa suala hilo hasa baada ya klabu kadhaa ikiwamo AS Vita ya DR Congo kupeleka malalamiko Shirikisho la Soka Afrika (CAF)? Endelea naye upate majibu kamili...!

ANAIONAJE YANGA?

“Sipendi sana kuiongelea Yanga, lakini tathmini yangu ni kwamba Yanga ni timu nzuri, nionavyo inaweza kuwa na wachezaji 11 wa kuanza, ila sina uhakika kama ina idadi kubwa ya wachezaji wa akiba.

“Huo ndio wasiwasi wangu wanaweza kufanya kazi na wachezaji 11 wa kikosi cha kwanza ambao ni wazuri na wenye ushindani, ila sioni kama wana kikosi kipana.

“Ninaposema kikosi kipana namaanisha kwamba unaweza kuwa na wachezaji wengi wazuri, lakini vipi ikitokea unamkosa mtu kama Yondani (Kelvin) hautapata shida? Ukimkosa Lamine (Moro) hautapata shida? Ukimkosa Tshishimbi (Papy) hautapata shida?

“Kama unavyojua kwenye soka kuna wakati kuna majeruhi na changamoto nyingine, ila wana wachezaji wazuri sana, siwezi kusema Yanga wana timu mbovu na yeyote akisikia anasema hivyo, atakuwa anaongea kishabiki.

“Unajua unapofanya usajili angalia timu yako uliyokuwa nayo mwaka jana na ile unayoisajili msimu huu, pia ujue wanalingana au wanazidi, sasa Yanga wajipime wapya walioingia ni wangapi wanalingana au kuwazidi wale waliotoka, kuna wachache walioingia ni wazuri sana kuna wengine sijaona wakicheza kabisa, hivyo kuna wakati inakuwa vigumu kufanya tathmini kamili.”

TUHUMA ZA KUPULIZA DAWA VYUMBANI?

“Hayo ni maneno tu, nasema ni maneno kwa sababu hizi kelele zilianzishwa na AS Vita, wenyewe walipokuja hapa, nafikiri walidanganywa na hawa watu wa Yanga, walipofika hotelini kwao hata chakula walikuwa hawali pale, wanajua wao wenyewe walikuwa wanapika wapi, magari walijitafutia wenyewe, walipokuja katika kikao cha mwisho cha mchezo (pre match meeting) wakaomba wapewe funguo za vyumba mapema.

“Yule mratibu wa mechi kutoka Cape Verde alivyokuwa mkali kwetu utasema alikuja pamoja na AS Vita, alikuwa anawasikiliza Vita karibu kila kitu wanachosema walikuwa wanaongea lugha moja ya Kifaransa. Saa sita na nusu mchana alienda mwenyewe uwanjani akakagua uwanja mpaka vyumba akienda na watu wa Vita,” anasema na kuongeza:

“Vita walipokuja uwanjani wakawa wamevaa vitu vya kinga wasivute hewa mbaya (mask), pia wakagoma kuingia kwenye vyumba, sasa Simba inahusika na hujuma gani hapo?

“Kama wameingia vyumbani saa sita mchana hizo dawa tumepuliza muda gani na vyumbani humo hawakuingia walikaa kwenye varanda, tukawafuata tukawaambia tuwapatie vyumba vingine hawataki, tubadilishane basi waje kwetu wakagoma kule kwetu kuna vyumba vingine tukawaambia waende kule wakagoma.

“Sasa dawa tulipuliza saa ngapi? Ile mechi yenyewe hebu kumbukeni jinsi Vita walivyocheza walionyesha kuchoka? Ile mechi mwishoni kila kocha alijilipua kwa kutumia mbinu za mwisho za kushambulia.

“Vita walitoka kutukosa bao, Manula (Aishi) akadaka na kuanzisha haraka tulipofika langoni kwao tukawafunga, sasa hizo dawa zilipulizwa lini?

“Kilichokuwa kimejengeka na miongoni mwa wachezaji, wapenzi na kila mtu ni kwamba timu yoyote ikija Uwanja wa Taifa lazima ifungwe, unajua kila kitu unachofanya kinaanzia katika akili yako unavyoiandaa.

“Niamini mimi ile idadi ya mashabiki si kitu kidogo kucheza na timu yenye mashabiki wengi vile na kelele zote zile zinakuzomea wewe sio kitu chepesi kaka.

“Bahati yao pale Taifa kuna ile sehemu ya riadha ingekuwa ni uwanja ule wa soka halisi mpira unachezwa pale mashabiki wako hapo tena 60,000, mfano Simba wajenge hata wa 45,000 tu utapigiwa kelele mpaka utakimbia na hapo utafungwa tu.

“Tuachane na Vita tuwaangalie Nkana nao tuliwapiga dawa? Nakumbuka kuna dakika za mwisho kabla hatujafunga bao la tatu, walitukosakosa mabao mengi sana kama mnakumbuka, yule kocha wa Nkana aliingiza viungo kama watatu hivi walitusumbua sana, mpaka kocha wetu alipoamua kuingiza viungo na sisi ndipo tukaanza kutawala mchezo na kuja kupata bao sasa hizo dawa tunapuliza wapi.

“Tuhamie kwa Al Ahly nakumbuka tulifunga bao dakika ya 68 baada ya hapo walitushambulia mpaka dakika ya mwisho, sasa unajiuliza hizi dawa zinapuliziwa wapi maana labda tungekuwa tunacheza na timu iko hoi hapo ungesema lisemwalo lipo,” anasema.

KELELE HIZO ZILIWASUMBUA?

“Zilisumbua sana tu. Nakumbuka Vita waliandika barua CAF, nao wakatuandikia barua kwamba kuna hizi taarifa zinaenezwa juu yenu, tukawaeleza ukweli, kwanza hawa walikuja na masharti yao yote kuanzia wakati wa mkutano wa mchezo (pre match meeting) tukawapatia tuliwaeleza yote, mwisho wa siku CAF waliwapuuza tu.

“Ni dhana tu ilijengwa bila kuwa na ushahidi wowote na nafikiri hili lilipata nafasi sana baada ya sisi kuwa tukienda nje tunafungwa. kufungwa kwetu kulitokana na kocha alikuwa hana mbinu sahihi za mechi za ugenini,” anafafanua Magori.

“Kuna maeneo tulikuwa tunafanya makosa sana unaenda uwanja kama wa Kamanyora wanaoutumia Vita unachezaje soka la kushambulia pale, Raja Casablanca akienda pale anakula tatu, sisi Simba itakuwaje?

Usikose kuendelea na Magori kesho Jumanne akieleza kitu gani kinakwamisha soka la Tanzania lisisonge mbele, sambamba na kuanika juu ya Friends of Simba kama bado lipo ama? Bila kusahau kufafanua kama amewahi kushiriki kuhujumu timu nyingine ili kuinufaisha Simba.

Itaendelea.