Luis, Bocco mzigo ule ule

ACHANA na sare ya juzi dhidi ya Mtibwa Sugar katika mechi yao ya pili ya Ligi Kuu Bara, unaambiwa nyota wa Simba wakiwamo, Luis Miquissone, John Bocco na Clatous Chama wataendelea kula shushu kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Ndio, klabu tano kati ya 18 zinazoshiriki ligi ya msimu huu, zinaonekana kuwa vizuri kiuchumi, huku Simba ikisisitiza itaendelea kuwatia mzuka nyota wake kwa bonasi kama iliyokuwepo msimu uliopita.

Mbali na kina Luis na Chama kunufaika na bonasi zao ndani ya Msimbazi, lakini nyota wa klabu za Namungo, Gwambina, Azam na Yanga nao wamewekewa mizigo ya maana mezani kwa ajili ya kuwatia morali wa kusaka matokeo uwanjani, japo viwango vinatofautiana.

Habari kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa, mabosi wa klabu hiyo hawajafanya mabadiliko yoyote ya viwago vya posho za bonasi kwa nyota wake katika Ligi Kuu ya msimu huu. Msimu uliopita Simba ilikuwa ikitoa zaidi ya Sh 10 milioni kwa wachezaji wake ili waganawe katika mechi wanazoshinda huku mgawanyo ulitofautiana kati ya wachezaji walioanza kikosi cha kwanza wakaa benchi mpaka wale wanaoishia kuwa wapenzi watazamaji jukwaani.

Ndani ya Simba, wachezaji waliocheza mechi husika na kushinda wanalipwa kati ya Sh 400,000 na 500,000 wakati wale walioishia benchi wanalipwa kati ya Sh 200,000 na 300,000 huku wanaoishia jukwaa hulipwa kati ya Sh 100,000 na 150,000 kutegemea na mechi.

Mmoja wa viongozi wa Simba aliyeomba kuhifadhiwa jina, alisema viwango vimebaki kama vilivyo, huku pia hata bonasi ya mechi yao ya Yanga, itaendelea kuwa kubwa zaidi kwani kwenye msimu uliopita ilikuwa dola 100,000 (zaidi ya Sh 200milioni) wanaposhinda.

“Hata hivyo, mfumo huu wakitoka droo ama kupoteza hakuna bonasi yoyote inayotolewa,” alisisitiza kigogo huyo.

Kwa upande wa Yanga msimu uliopita walikuwa wakitoa Sh 10 milioni kwa ajili ya bonasi ingawa inadaiwa msimu huu dau lao limepanda ila wachezaji wanapaswa kujituma zaidi kwani wakitoka sare ama kupoteza basi hawapewi kitu.

Hata hivyo hakuna kiongozi wa Yanga aliyeweza kuweka bayana, kwani mmoja wa watu wa Kamati ya Mashindano alisema bonasi hiyo ilikuwa haijapangwa rasmi, lakini taarifa za ndani zinasema kila kitu kimeshawekwa sawa, ila ni siri ya klabu.

Nao Azam FC ambao bonasi yao haipo wazi hutoa kwa mechi ambazo wameshinda na droo.

“Sare ya nyumbani haina bonasi ila ushindi, lakini sare na ushindi ugenini kuna bonasi, yote hiyo ni kuwapa motisha wachezaji kufanya vizuri,” alisema Ofisa Habari wa timu hiyo Zaka Zakazi. Habari kutoka ndani ya Namungo FC, zinasema hutengwa Sh 1,500,000 milioni.