Liverpool wanateseka hawa wamebeba kiulaini

LONDON, ENGLAND

WAKATI mwingine maisha huwa hayatendi haki. Cheki mastaa matata kama Steven Gerrard na Gianfranco Zola wametamba sana Ligi Kuu England, lakini hakuna hata mmoja aliyefanikiwa kubeba taji hilo. Liverpool inasumbuka kwa miaka kibao tangu ligi hiyo ilipoanza, licha ya kuwa na mastaa kibao kwenye kikosi chao, wameshindwa kubeba taji hilo.

Lakini, utashangaa kuna wachezaji hao wa kawaida sana wamewahi kushinda taji hilo. Kweli wakati mwingine unahitaji kuwa na bahati kushinda ubingwa. Ndiyo hivyo, hawa wamebeba ubingwa wa Ligi Kuu England.

5. Jeremie Aliadiere (Arsenal)

Jeremie Aliadiere alikuwa kwenye kiksoi cha Arsenal kwa miaka sita, lakini muda mwingi alikuwa kwenye benchi tu. Straika huyo alifunga bao moja tu katika mechi 29 alizochezea Arsenal ile iliyokuwa chini ya Arsene Wenger.

Lakini, mchezaji huyo alikuwa na bahati ya kushinda taji la Ligi Kuu England katika msimu wa 2003-04 na msimu huo alicheza mechi 10 tu, huku mechi nyingi alizocheza tayari Arsenal ilikuwa imeshajihakikishia ubingwa.

4. Alexander Buttner (Man United)

Alex Buttner alisajiliwa na Manchester United mwaka 2012 na alikwenda kucheza mechi 13 tu katika klabu hiyo yenye maskani yake Old Trafford. Msimu huo wa 2012/13, ambao Man United ilibeba ubingwa wa Ligi Kuu England, Buttner ndio aliocheza mechi 13 na kupata medali hiyo ya ubingwa wa ligi. Beki huyo wa Kidachi aliondoka Man United kwenda kujiunga na Dynamo Moscow mwaka 2014 na sasa anacheza Jong Vitesse.

3. Mateja Kezman (Chelsea)

Chelsea walimnasa Mateja Kezman kipindi hicho alipokuwa kwenye ubora wake huko PSV na alifunga mabao 129 katika mechi 176. Lakini, nyakati zake Stamford Bridge zilikwenda kuwa ngumu ndani ya uwanja licha ya kwamba hakuondoka hapo mikono mitupu. Kezman alifunga mabao manne tu katika mechi 25, lakini aliachana na Chelsea akiwa amebeba ubingwa wa Ligi Kuu England kabla ya kuondoshwa kikosini, akitimka zake Atletico Madrid.

2. Juan Cuadrado (Chelsea)

Mchezaji mwingine wa Chelsea aliyekuwa na bahati ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England, wakati wengine kama Liverpool wanasoka kwa miaka kibao bila ya kuonja utamu wa kubeba taji hilo ni Juan Cuadrado.

Staa huyo wa Colombia, alinaswa na Chelsea kwa ada ya Pauni 24 milioni akitokea Fiorentina mwaka 2014. Cuadrado hakuwa na wakati mzuri Chelsea, akicheza mechi 12 tu katika msimu wake wa kwanza, lakini alibeba ubingwa wa Ligi Kuu.

1. Jack Rodwell (Man City)

Kinda wa Kingereza, Jack Rodwell wakati anakua wengi waliamini kwamba angekuwa kitu kikubwa sana kwenye soka la nchi hiyo.

Lakini, Jack Rodwell alishindwa kukitendea haki kipaji chake, majeruhi mfululizo yalimkwamisha kwenye kutimiza ndoto zake.

Hata hivyo, mwaka 2012 alipata bahati ya kusajiliwa na Manchester City, ambayo ilikwenda kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England msimu wa 2012/13 na hivyo Rodwell kupata medali ya ubingwa huo.