‘Kubwa kuliko' ndio imemng'oa Zahera

Wednesday November 6 2019

‘Kubwa -kuliko' - imemng'oa -Zahera -Yanag SC-Jangwani-kocha-wanayanga-mwenyekiti-Mshindo-Msolla-

 

By Luqman Maloto

MWINYI Zahera sio kocha wa Yanga tena. Imeamuliwa na wafanya uamuzi wa Jangwani. Kwao imewapendeza kumfurusha kocha huyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Kwa nini Zahera ametimuliwa? Kabla ya kujibu swali, tukumbuke msimu uliopita ulivyonakshiwa na ufalme wa Zahera Yanga.

Yanga ilipitia wakati mgumu mno. Timu ikaendeshwa kwa donee. Bakuli lilipitishwa nchi nzima chini ya jina “Saidia timu ya wananchi”. Zahera alikuwa kocha, mlezi wa wachezaji, mdhamini na mhamasishaji. Alikuwa hamasa ya wachezaji kujituma licha ya nyakati ngumu walizokuwa wanapitia. Maisha ya bila uhakika wa malipo ya mshahara, posho wala matibabu mchezaji alipoumia.

Ni nyakati ambazo mashabiki waliikumbatia Yanga kwa sababu ya Zahera. Walitoa michango ya hali na mali kwa sababu walijenga imani na Zahera. Ikaelezwa Zahera sio tu aliidai Yanga malimbikizo ya malipo yake, bali pia alitumia fedha zake kuendesha timu.

Mashabiki wangeambiwa nini kwa Zahera? Wanayanga hawakutaka kusikia chochote kutoka kwa viongozi. Vile jitihada za kumrejesha Yusuf Manji ziligonga mwamba, Zahera akawa kila kitu. Unaanza vipi kumpinga Zahera wa 2018-2019?

Zahera alimtoa nduki aliyekuwa meneja wa timu, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, mtu kipenzi sana cha Wanayanga. Zahera alimtimua golikipa lulu Yanga, Benno Kakolanya, kwa sababu za ovyo. Nani wa kumpinga Zahera? Ungethubutu ungekutana na hasira za mashabiki. Wenye Yanga yao.

Advertisement

USPESHO WA ZAHERA 2018-2019

Ukitazama matokeo ya Yanga 2018-2019, yalikuwa mazuri, tatizo walikutana na Simba (wapinzani wao wa jadi), waliokuwa katika kiwango Bora kabisa. Yanga ilimaliza msimu ikiwa na pointi 86, nyuma ya Simba iliyofikisha pointi 93. Yanga ilishinda michezo 27, ikadroo mitano, ikafungwa sita. Kwa wastani hayakuwa matokeo mabaya sana. Ilimaliza nafasi ya pili, mbele ya Azam iliyokuwa na kila kitu.

Yanga ilitolewa mashindano ya Shirikisho, ikaelekea kukosa nafasi ya kushiriki mashindano ya Kimataifa. Mpaka nafasi ya “Zali la mentali” ilipotoka CAF.

Kwa utamaduni wa soka la Tanzania, matokeo ya Yanga kuondolewa Kombe la Shirikisho na kumaliza nyuma ya Simba kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara misimu miwili mfululizo, ilitosha kuamsha manung’uniko na kelele.

Hali ilikuwa kimya na Zahera alitetewa aliipigania na kuivusha timu katika kipindi kigumu. Ndio sababu Yanga ilicheza mpira kwa utulivu. Zahera hakuwa na presha ya matokeo. Mazingira yalimfanya aone hakuwa na deni kubwa la kulipa.

“Hakuna cha kupoteza”. Zahera aliiongoza Yanga katika kipindi ambacho ilikuwa haina cha kupoteza. Hiyo ndio sababu ya utulivu mkubwa uliokuwepo.

UBOVU WA ZAHERA 2019-2020

Yanga haikujiandaa kucheza Klabu Bingwa Afrika, lakini ikapewa nafasi. Ikaitoa Township Rollers ya Gaborone, Botswana, ambayo ilipewa nafasi kubwa kuvuka hatua iliyofuata kuliko Yanga.

Simba ambayo ilijiandaa kiusajili na uwekezaji kwa jumla kwa mashindano ya CAF, ikiwa na kumbukumbu ya kufika robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika 2018-2019, ilitolewa mechi ya kwanza kwa iliyoonekana dhaifu, UD Songo ya Msumbiji.

Mpaka hapo, Zahera aliiwezesha Yanga pazuri, licha ya kutowekeza vizuri kiusajili na maandalizi mengine, dhidi ya Simba.

Yanga ikaondolewa na Zesco ya Zambia, timu ambayo uwekezaji wake ni zaidi ya Yanga. Baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa na Zesco, ikahamia Shirikisho CAF, ikakutana na Pyramids ya Misri ambayo iliitoa

Kwa kifupi ni kuwa matokeo ya Yanga kufungwa na Pyramids yalikuwa chagizo kwa timu kujipanga. Ilikutana na timu bora zaidi. Ni zuzu pekee anayeweza kuona sawa Yanga kufungwa na Zesco, halafu anune Yanga kutolewa na Pyramids. Wakati kiuhalisia, Pyramids wana timu bora zaidi ya Zesco. Tuje Ligi Kuu Bara, Yanga wameshacheza michezo minne, wameshinda miwili, sare mmoja na wamepoteza mechi moja. Simba wanaongoza ligi wakiwa wamecheza mechi 8, wameshinda saba na kufungwa moja.

Yanga wanadai mechi nne ili kuwa sawa na Simba. Mechi 4 ni pointi 12. Yanga sasa hivi wana pointi 7. Hivyo, kama wakishinda viporo vyote na ingekuwa ligi inasimama kupisha Yanga wamalize viporo, ingepanda mpaka nafasi ya pili kwa pointi 19. Simba ina pointi 21. Kwa wastani, Yanga haijafanya vibaya msimu huu. Imefungwa mechi moja ligi kuu, Simba pia imefungwa moja. Imedroo moja, Simba haijatoa sare. Kimatokeo Yanga si ya kitemea mate.

KWA NINI ZAHERA AMETIMULIWA?

Tujibu swali sasa; Yanga ya msimu uliopita iliingia kwenye mashindano ikijiona ni dhaifu. Zahera aliilea na akaachwa afanye atakavyo. Timu haikuwa na matarajio makubwa.

Yanga ya msimu huu ina matarajio makubwa. Uongozi mpya wa Yanga ulipita kwa ahadi kemkemu. Hivyo, viongozi waliopo madarakani wana deni la matarajio ya Wanayanga. Deni hilo, linategemea matokeo ya uwanjani. Lazima wamdai kocha. Juni 15, mwaka huu, Yanga walifanya harambee waliyoiita “Kubwa Kuliko”. Wanachama, mashabiki na wadau wa soka waliimwagia timu pesa. Fedha kiasi cha zaidi ya bilioni moja zilipatikana.

Jinsi Yanga ilivyofanya usajili wa kishindo, bandika bandua, ilikuwa gia ya uongozi, Mwenyekiti Mshindo Msolla na Makamu Mwenyekiti, Frederick Mwakalebela, kuwaonyesha wanachama na mashabiki kuwa upele ulipata mkunaji.

Jumlisha na fedha zilizokusanywa kwenye Kubwa Kuliko, bila shaka uongozi unaona unalo deni la kulipa. Uongozi unategemea timu iwalipie deni. Ni hapo lazima uongozi wa Yanga upeleke presha kwenye benchi la ufundi, ndio maana Zahera kang’olewa na safu nzima kasoro kocha wa makipa, Peter Manyika. Tuelewane sasa; kilichomwondoa Zahera Yanga sio matokeo mabaya ya timu, bali presha ya nyakati. Yanga ya msimu huu ina presha kubwa ambayo imekuwa vigumu kwa Zahera kuikabili.

Kingine, taa nyekundu ilikuwa imeshawaka. Dalili Zahera alikalia kuti kavu, zilishaonekana. Jinsi Zahera alivyokuwa analalamika uongozi hauhudumii wachezaji na fedha za Kubwa Kuliko zilitumika kwa namna ambavyo hakuridhika, ilitosha kuonyesha Zahera na uongozi Yanga walishashindwa kufanya kazi pamoja. Hivyo, uamuzi uliochukuliwa, ni wazi ulitabiriwa na wengi. Kwa hiyo tuseme; Yametimia!

Advertisement