Kompany agoma kurudi Etihad

MANCHESTER ENGLAND. VINCENT Kompany amegomea nafasi ya kurudi Manchester City kwenda kujiunga na benchi la ufundi na badala yake ameamua kubaki zake Anderlecht.

Gwiji huyo wa Man City na nahodha wa timu hiyo ya Etihad alipata ofa ya kurejea kwenye klabu kujimuika katika benchi la ufundi mwaka mmoja baada ya kuondoka.

Kocha Pep Guardiola amekuwa akitafuta msaidizi kuziba pengo la Mikel Arteta, aliyetimka kwenye kuchukua mikoba ya kuwa kocha mkuu kwenye kikosi cha Arsenal, Desemba mwaka jana. Kinachoelezwa ni kwamba mjadala ulifanyika na kujadili kama inafaa kumrudisha Kompany uwanjani Etihad kuziba pengo hilo la Arteta. Kwenye kikosi hicho, Kompany amekuwa na hazi kubwa baada ya kushinda mataji 10 katika miaka 11 aliyodumu na timu hiyo huku sehemu kubwa akiwa nahodha.

Hata hivyo, mapema wiki hii, Kompany aliithibitishia Anderlecht kwamba amejitolea kwa nguvu zote kubaki kwenye timu hiyo hadi mkataba wake utakapofika tamati 2022 na kuendelea. Ripoti zinadai kwamba moja ya sababu zinazomfanya Kompany agome kurudi Etihad kwa sasa ni kuhusu mpango wake wa kutaka kuendelea kucheza baada ya kuona majeruhi yamemharibia sana, kitu anaamini akirudi Man City hatapata nafasi ya kufanya hivyo.