Kocha wa Samatta ashtukia jambo

KOCHA wa Aston Villa, Dean Smith amesema alitazama kila dakika ya michezo yao iliyopita kwa lengo la kutatua makosa ambayo walikuwa wakiyafanya kabla ya Ligi Kuu England kusimamishwa kutokana na janga la corona (Covid-19).

Wachezaji wa Aston Villa, akiwemo nahodha wa timu ya Taifa la Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta walirejea wiki iliyopita kwa mara ya kwanza kushiriki mazoezi katika Uwanja wa Bodymoor Heath baada ya miezi miwili kupitia bila kukutana.

Smith alisema alitumia wakati huo ambao ligi ilisimama kuzichambua mechi zote huku akiwahusisha pia wachezaji wake kila mmoja kutumia video.

Aston Villa ambayo alijiunga nayo Samatta wakati wa dirisha la usajili la Januari akitokea KRC Genk, wapo nafasi 19 katika msimamo wa ligi baada ya kupoteza michezo mitano mfululizo kabla ya janga la corona.

Smith alisema: “Mimi sio mtu ambaye kwa kawaida hurudi na kutazama kila mchezo, lakini kwa wakati huu nimeangalia kila mchezo wetu kwa kweli kulikuwa na mambo ya kuchukua.

“Nimeweza kufanya marejeo ya video zetu za mechi zilizopita na kila mchezaji, ni jambo ambalo sidhani kama naweza kulifanya tena, lilichukua muda mwingi lakini ni kutokana na kusimama kwa ligi.

Wachezaji wa Aston Villa waligawanywa katika makundi manne na kila mmoja alikuwa akifanya mazungumzo ya kawaida na Smith na wasaidizi wake, na mwisho kufanya mikutano ya mbinu kila baada ya siku tatu.

“Tulikuwa na mazungumzo na wachezaji ambayo yalitakiwa kudumu kwa dakika 45, lakini ikaishia kuwa saa na nusu,” alisema na kuongeza:

“Yalikuwa mazungumzo marefu na mazuri na wachezaji ambao ni wazi kuwa, hautapata nafasi ya kufanya nao tena. Kwa tunajua ni nini tunapaswa kufanya ili kuwa bora.”