Kocha mpya KMC akunjua makucha

Tuesday January 14 2020

 

By Majuto Omary

Dar es Salaam. Kocha mpya wa KMC Haruna Harerimana amewataka wachezaji wake kucheza kwa malengo ili kuipa mafanikio klabu hiyo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Harerimana alisema anataka wachezaji wanaojituma ambao watacheza kwa malengo ya kuisaidia KMC katika Ligi Kuu.

Kocha huyo wa zamani wa Lipuli alisema atafanya kazi KMC na amewataka wachezaji kuonyesha vipaji vyao ili kumaliza ligi wakiwa katika nafasi nzuri.

“Nimefurahi kupata uongozi ambao unajali maslahi ya wachezaji na watendaji wa timu. Jambo la msingi naomba ushirikiano wa wachezaji wote ili tufikie malengo,” alisema Harerimana.

Mbali na kumnasa kocha huyo ambaye ataziba pengo la Etienne Ndayiragije, KMC imewaondoa wachezaji watano Aaron Lulambo, George Sangija, Rehani Kibingu, Melly Mongolare na Janvier Bokongu. Pia Vitalis Mayanga ameuzwa Ndanda ya Mtwara.

Mwenyekiti wa Bodi ya KMC, Meya Benjamini Sitta alisema Harerimana ametia saini mkataba wa miezi 18 baada ya kufanyika mchujo wa makocha walioomba nafasi hiyo.

Advertisement

Advertisement