Kocha mpya Alliance aanza na mabeki

Muktasari:


Uongozi wa timu hiyo yenye maskani yake jijini hapa ulifanya mabadiliko la benchi la ufundi kwa kumrejesha kikosini Mzirai huku Fred Felix Minziro ikielezwa atapangiwa majukumu mengine.

KOCHA wa Alliance FC, Kessy Mzirai amesema baada ya kukabidhiwa jukumu la kukinoa kikosi hicho kazi ambayo anaifanya sasa ni kuboresha safu ya ulinzi ambayo ina na mapungufu makubwa.
Uongozi wa timu hiyo yenye maskani yake jijini hapa ulifanya mabadiliko ya benchi la ufundi kwa kumrejesha Mzirai huku Fred Felix Minziro ikielezwa atapangiwa majukumu mengine.
Mzirai alisema ameanza mazoezi na kikosi hicho na lengo lake kubwa ni kuhakikisha wanarekebisha mapungufu mbalimbali hasa eneo la ulinzi.
Alisema mabeki wake katika mechi za ligi kuu walizocheza hivi karibuni wamekuwa wakiruhusu mabao rahisi jambo ambalo analifanyia kazi kwa sasa kwani anataka kasoro hizo zimalizike.
“Nafanyia kazi zaidi eneo la ulinzi kwani tumekuwa tukiruhusu sana mabao ya kizembe ambayo kama kungekuwa na umakini basi yangeweza kuzuilika,” alisema Mzirai.
Kocha huyo alisema anajua jukumu zito alilonalo kwasasa la kuhakikisha timu hiyo inabaki kwenye ligi msimu ujao kitu ambacho anatakiwa kukomaa nacho.