Kiba bado kidogo tu unaambiwa

Muktasari:

Mshambuliaji wa Coastal Union, Ali Kiba ameanza mazoezi kidogo kidogo na wachezaji wenzake baada ya kukosekana katika kikosi hiko kwa muda mrefu kutokana na majukumu yake ya nje ya uwanja yaliokuwa yanamkabili.

MASHABIKI wa soka wameshaanza kusahau kama Coastal Union ilimsajili Ali Kiba kwa vile mchezaji huyo hawajawahi kukaa japo benchi katika mechi za Ligi Kuu Bara, lakini sasa mashabiki hao wajiandae kwani kamaa bado kidogo tu kuliamsha.
Kiba mmoja ya nyota wa muziki wa kizazi kipya ameanza kujifua na wenzake baada ya kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na kukabiliwa na majukumu mengine ya kisanii, lakini Kocha wake JUma Mgunda amewatuliza mashabiki.
Mgunda alisema Kiba amerejea upya kikosini akiwa ameanza kujifua na wenzake tayari kuanza kuwasha moto katika Ligi Kuu.
“Hajaja kuanza upya kwani alikuwa anafanya mazoezi binafsi hivyo anapokuwa na wenzake na kupata programu maalumu itamsaidia kukaa vizuri zaidi na tutaanza kumtumia muda si mrefu ili kutuliza mzuka wa mashabiki wanaotaka kumuona,” alisema.
“Huyu alikuwa na mikataba nje ya uwanja, hivyo kwa sasa amerejea upya , mashabiki watarajie kumuona uwanjani na timu yake kwani muda wa kucheza sasa anao."
Hata hivyo kauli ya Kocha Mgunda sio ya kwanza, kwani hata awali alishawapa tumaini mashabiki ya kuanza kumtumia Kiba, lakini mpaka ligi ikiingia raundi ya 14 supastaa huyo hajawahi kucheza wala kukaa benchi la akiba la Wagosi wa Kaya.