HISIA ZANGU : Kakolanya, hadithi ya Muosha huoshwa na mengi mengineyo

Muktasari:

  • Jambo hili lina maana nyingi tofauti. Kwanza kabisa ni hadithi ya Muosha Uoshwa. Kakolanya ana haki zote za kuvunja mkataba wake kwa mujibu wa sheria za soka. Kuanzia kwa wazungu mpaka huku TFF. Kuanzia sheria za kazi za Ulaya mpaka za Tanzania.

HALI tete Jangwani. Nilisikia kipa, Beno Kakolanya kavunja mkataba. Baadae ikasikika Kakolanya bado yupo yupo kidogo. Hata hivyo, tatizo la msingi linabakia pale pale.avunje mkataba au asivunje, hajalipwa mshahara wake wa miezi mitano.

Jambo hili lina maana nyingi tofauti. Kwanza kabisa ni hadithi ya Muosha Uoshwa. Kakolanya ana haki zote za kuvunja mkataba wake kwa mujibu wa sheria za soka. Kuanzia kwa wazungu mpaka huku TFF. Kuanzia sheria za kazi za Ulaya mpaka za Tanzania.

Mara ngapi tunawalaumu wachezaji wa Kitanzania kwa kutojituma? Mara nyingi tumefanya hivyo. Wachezaji wanalelewa na mpira halafu hawajitumi. Sasa tumeingia katika kesi ambayo mchezaji anaitumikia klabu lakini halipwi. Muosha uoshwa.

Kama ambavyo tunawalaumu wachezaji wa kutojituma basi ndivyo tunavyowalaumu Yanga kwa kutomlipa mchezaji.

Beno ana haki zote za kuvunja mkataba wake kwa sababu tuliachana na siasa za Ujamaa na kujitegemea miaka mingi iliyopita.

Kama akiamua kutumia busara, sawa. Kama akiamua kuvunja mkataba asilaumiwe.

Zama za Ujamaa na kujitegemea zilipita muda mrefu. Huo ni ukweli ingawa katika hali halisi ningependa Beno abakie Yanga. Hii ni kwa sababu moja tu, ni kipa wa kiwango cha juu ambaye anaichezea timu yetu ya taifa.

Akienda Simba au Azam haitakuwa vema sana kwa sababu tayari kuna makipa wa kudumu katika timu hizo na kiwango chake kitafifia kiasi kwamba tutampoteza kipa mahiri wa timu ya taifa.

Siku hizi kama Aishi Manula akiumia katika lango la Taifa Stars tunapata moyo tukimwona Beno anapasha misuli yake moto.

Tukiachana hilo, suala la Beno linakuja na maana nyingine. Nyuma ya pazia Yanga wanavuna kila walichokipanda.

Tajiri wao aliyepita ‘alitanua’ goli la mishahara. Wachezaji wengi walikuwa na mishahara mizuri. Kwa sasa mishahara hiyo inawapa tabu.

Tatizo hawakujiandaa kuishi bila ya yeye. Walipaswa kumwomba awaachie mipango ya muda mrefu ya kumudu maisha bila ya yeye. Yanga walikuwa wanafurahia keki ya muda. Walau wangeomba Andazi la kudumu.

Sio kwamba Yanga hawapendi kumlipa Beno. Hapana. Wanapitia nyakati ngumu kwa sababu ukiwapelekea wanachama wa kawaida dau la mshahara wa miezi mitano la Kakolanya, ukijumlisha na pesa ya usajili anayodai, nadhani wengi hawataamini.

Hii sio kwa Kakolanya pekee. Ipo kwa wachezaji wengi wa Yanga ambao walipewa mikataba wakati wa utawala ule.

Sawa, timu ilikuwa inaonekana ya kitajiri, mara ipo Uturuki, mara ipo hewani kuliko ardhini, lakini hakukuwa na mipango endelevu.

Suala hili la Beno linaingia katika swali jingine. Hawa waliochukua fomu Yanga wanajua wanachokifuata klabuni?

Nilitamani kuandika mjadala huu siku zijazo, lakini baada ya suala la Beno ni vema kuulizana sasa hivi. Wanajua wanachokigombea? Kwa taarifa yao wanagombea mambo matatu.

Kwanza kabisa wanagombea kulipa madeni ya sasa ambayo yanawakabili katika maeneo mbalimbali. Eneo moja ni hili hapa la Beno.

Kuna wachezaji wengi ambao wanadai kama ilivyo kwa Beno. Hawadai pesa kidogo, wanadai mishahara ya miezi mingi kama ilivyo kwa Beno.

Pili baada ya kulipa hiyo mishahara inabidi waunde kikosi chenye hadhi ya Yanga kama kile kikosi cha kina Donald Ngoma.

Tatizo la mwenyekiti wa wakati ule aliweka kiwango ambacho kwa kilitakiwa kwa Yanga. Wachezaji wenye ubora, kiwango chenye ubora. Tatizo mambo haya hayaji bila ya pesa. Wamejiandaa na pesa?

Wakati mwingine suluhisho sio pesa tu, bali ni mipango ya pesa. Wana suluhisho la mipango ya muda mrefu kuhusu pesa?

Tunaimba Yanga na Simba zina rasilimali za kuwa timu kubwa, lakini kuongea ni jambo moja, kutenda ni jambo jingine.

Je na wao wakiachana na Yanga wataiacha kama walivyoikuta au wataiacha ikiwa na uwezo wa kipesa wa kulipa mishahara ya akina Beno wengine?

Hili ndio tatizo kubwa ambalo limekuwa likiwakabili Yanga na Simba kwa miaka mingi.

Leo ghafla Mohamed Dewji akighairi kila anachofikiria kuhusu Simba unaweza kusikia kesho Simba ina madeni kuanzia ya hoteli mbalimbali hadi ya wachezaji. Kwa nini hatuna mipango endelevu na ya muda mrefu?