Kakolanya, Shilton wasilete makundi Simba SC

Thursday June 25 2020

HIVI karibuni kumeibuka msuguano baina ya kipa Beno Kakolanya na kocha wake Mwarami Mohamed ‘Shilton’ baada ya kipa huyo kukosa nafasi ya kucheza kutokana na kocha wake kudaiwa kumtamkia kuwa ameshuka kiwango na hivyo atakuwa kipa namba tatu wa Simba.

Imeelezwa kwamba Shilton amempa nafasi Aishi Manula kuwa kipa namba moja huku Ally Salim akichukuwa nafasi ya Kakolanya ya kukaa benchi kama kipa chaguo la pili , huku Kakolanya ambaye alikuwa chaguo la kwanza katika klabu aliyoihama ya Yanga, sasa amekuwa mtu wa kukaa jukwaani.

Kakolonya si kwamba hajawahi kupata nafasi katika kikosi cha kwanza Simba. Msimu huu amecheza jumla ya mechi tisa zikiwemo mechi mbili za Kombe la Shirikisho na saba za Ligi Kuu Bara.

Simba wamecheza mechi 31 hadi sasam sasa ambapo kati ya mechi hizo, Manula amecheza mechi 22 za Ligi Kuu huku pia akidaka baadhi ya mechi za Kombe la Shirikisho linalodhaminiwa na kituo cha runinga cha Azam.

Shilton ni kocha wa makipa ambaye amekaa ndani ya Simba kwa zaidi ya miaka miwili. Anawafahamu vyema makipa wake na kwamba nani awe kipa namba moja, mbili na tatu.

Kati ya makipa hao watatu, hakuna kipa ambaye hana udhaifu kwani kuna wakati hata Manula alikuwa akilalamikiwa kushuka kwa kiwango hasa pale baada ya kuruhusu mabao mawili ya mahasimu wao Yanga katika sare ya 2-2, mechi ambayo Simba walitangulia kwa kuongoza kwa mabao 2-0 Januari 4, mwaka huu.

Advertisement

Manula alianza msimu kwa kuaminiwa kama kipa chaguo la kwanza. Lakini baada ya sare ile dhidi ya Yanga mashabiki walianza kuimba “tunamtaka Kakolanya” wakionyesha kutoridhishwa na kiwango cha Manula.

Bao la shuti la mbali la Mapinduzi Balama na la kichwa la Mohamed Issa ‘Banka’ yalimponza Manula akapoteza namba moja kwa Kakolanya.

Mashabiki walimtuhumu Manula kwamba ana udhaifu wa kufungwa mashuti ya mbali kwamba la Balama halikuwa la kwanza. Akapoteza namba kwa Kakolanya.

Wataalamu wengi wa soka wakiwemo makocha na wachambuzi walizungumzia kiwango cha Manula kwamba ana makosa yanayojirudia anapokuwa golini jambo ambalo walimsihi alifanyie kazi ili uwezo wake uonekane kuwa bora zaidi.

Ni kipa huyo huyo anayefundishwa na Shilton, alikaa kwa muda nje ya uwanja na aliporejea alipata nafasi ya kucheza. Wakati yupo nje, Kakolanya ndiye aliongoza jahazi ambapo katika mechi alizocheza aliruhusu mabao sita.

Inawezekana kweli kiwango cha Kakolanya kimeshuka hadi kutupwa kuwa kipa namba tatu kuchukuwa nafasi ya Salim ambaye amepanda namba mbili, lakini huenda mapokeo ya jambo hilo yamekuwa tofauti ndiyo maana kumekuwepo na sintofahamu.

Mapokeo ya jambo hilo kwa Kakolanya kuonekana kuwa tofauti hadi kusababisha kocha mkuu Sven Vandenbroeck kuingiliana kati ni namna kocha Shilton alivyoliwasilisha kwa mchezaji wake. Uwasilishwaji wa jambo unaweza kupokewa kwa namna tofauti.

Kuna haja ya viongozi kuwaandaa wachezaji wao kisaikolojia namna ya kupokea taarifa binafsi kuhusu utendaji wao kazi. Inaonekana bado hakuna utayari wa mapokeo kwa kila mmoja, na inaleta picha tofauti kwa watu walio nje ambao waamini kuwa kuna tatizo ya kibinafsi baina ya wawili hao.

Hii pia inatokana na taarifa ambazo zinatajwa kutoka ndani ya timu hiyo juu ya wawili hao kwamba hakuna maelewano mazuri katika utendaji wao wa kazi.

Kama ni kweli, basi kuna haja na kila sababu ya viongozi kuwaweka sawa wawili hao maana lengo lao ni kujenga Simba moja na sio Simba ya makundi ama ya kuona baadhi ya wachezaji ni bora kuliko wengine.

Hii italeta madhara ndani ya timu, kwani hakutakuwapo na ushirikiano mzuri wa kuipa mafanikio Simba kama makocha wanatengeneza makundi ya wachezaji fulani waonekane bora kuliko wengine.

Ni kweli ishu ya nani acheze si jukumu la mchezaji bali ni kocha mwenyewe lakini hii ya Kakolanya inategemea na namna inavyoendelea maana taarifa zinaonyesha kuwa tofauti na yale yanayoendelea ndani ya timu hiyo.

Advertisement