Kagere amtikisa straika Yanga

MASHABIKI wa Simba kwa sasa wanapiga sana kelele mtaani juu ya chama lao, wakihesabu siku tu kabla ya kuona ndoo ya Ligi Kuu Bara ikitua Msimbazi kwa msimu wa tatu mfululizo, lakini mpango unaosukwa ili kumbeba Meddie Kagere, umemtikisa nyota wa zamani wa Yanga.

Kagere, ambaye anacheza soka kwa msimu wa pili akiwa na Simba iliyomsajili kutoka Gor Mahia ya Kenya, ndiye kinara wa mabao katika Ligi Kuu akiwa ametupia mara 19 na akiifukuzia tuzo ya pili mfululizo ya ufungaji bora akitaka kuandika rekodi mpya nchini.

Rekodi zinaonyesha haijawahi kutokea Mfungaji Bora wa Ligi Kuu kuitetea tuzo yake, lakini kwa mabao aliyonayo na mipango inayodaiwa kusukwa ili kumrahisisha Mnyarwanda huyo mwenye asili ya Uganda kutwaa tuzo na kuvunja rekodi ya Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ ya 1999.

Katika msimu huo, Mmachinga alifunga jumla ya mabao 26 ambayo hajawahi kufikiwa na straika yoyote kwa zaidi ya misimu 20, lakini Kagere amesaliwa na mabao nane tu ili kuipita na kuandika rekodi mpya, lakini kampeni hiyo ya Msimbazi imemshtua nyota huyo wa zamani.

Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola na baadhi ya nyota wa klabu hiyo walinukuliwa mapema wiki hii kwamba, wanataka kuona wanatetea ubingwa wa Bara kwa msimu wa tatu, pia watahakikisha Kagere ananyakua tena tuzo ya Mfungaji Bora kupitia mechi 10 zilizosalia sasa.

Akizungumza na Mwanaspoti jana, Mmachinga aliyewahi kukipiga Bandari Mtwara kabla ya kutua Yanga na baadaye kuhamia Simba, alisema anajisikia fahari kuendelea kuwa Mfungaji Bora kwa muda mrefu sasa, lakini ameshtushwa kusikia eti Kagere anatengenezewa mikakati ya kuifikia ama kuivunja rekodi yake.

Msimu uliopita, Kagere alifunga mabao 23 na kushindwa kuipiku rekodi hiyo ya Mmachinga na nyota huyo wa zamani wa Yanga alisema, hata kama atapitwa rekodi yake, anajivunia kwa vile itavunjwa na nyota wa kigeni, lakini pia wakati akiiweka mechi zilikuwa chache kuliko sasa.

Mmachinga alisema kinachomfurahisha ni kuona jinsi gani timu zinakuwa na mpango mkakati wa kuivunja rekodi yake, ilihali wakati akicheza na kuiweka hakukuwa na mipango ya hila kama hiyo na pia alicheza kwenye mazingira magumu na yenye timu ngumu tofauti na ilivyo kwa sasa.

Alifafanua, enzi akiichezea Yanga na kuweka rekodi hiyo wakati Yanga ikibeba ubingwa na Kombe la Kagame nchini Uganda, huku wakiukosa ubingwa wa Bara kwa tofauti ya alama tatu nyuma ya Mtibwa walionyakua taji, hakudhani idadi ya mabao aliyofunga yataweka rekodi inayodumu mpaka sasa na kuumiza vichwa wachezaji wengi.

Alisema, alikuwa anafunga mabao kwa ‘muvu’ za kawaida na nyingine akipasua ukuta na wala hakukuwa na mikakati ya kuandaliwa mazingira ya kuwa mfungaji bora na alichangia zaidi ya nusu ya mabao ya timu yake iliyomaliza na 44 katika mechi 30 tu, kwani timu zilikuwa 16.

“Wachezaji walikuwa wanacheza mechi ya kutafuta ushindi na wala haikupangwa kuwa lazima mimi nifunge, zawadi kubwa wakati huo ilikuwa kutwaa ubingwa na mahesabu yalikuwa kwenye pointi na mabao ya kufunga,” alisema straika huyo aliyetamba pia na Taifa Stars na kuongeza;

“Hali hiyo ilitufanya wachezaji wa Yanga kuzitumia nafasi zote za kufunga na hata kwenye suala la penalti, sikuwa mpigaji, kulikuwa na wachezaji wanaopiga na hata kama ilitokea, basi si kwa mpango maalum, hivyo nastaajabu taarifa za Kagere kutaka kubebwa kijanja,” alisema.

Nyota huyo alikiri amemsikia Matola akisema jinsi gani wao wameweka mikakati ya kuhakikisha Kagere anakuwa mfungaji bora, mbali na kutetea ubingwa kwa msimu wa tatu.

“Kumbe kuna wafungaji bora wa kutengenezwa, mimi sikuwa hivyo, hata ukiwauliza wachezaji wenzangu wa enzi zile, watakujibu hakukuwa na mpango huo, kwani hakukuwa na ushindani katika nafasi hiyo zaidi ya kuandikwa na vyombo vya habari kushinda kiatu cha dhahabu.”

“Kwa kifupi, hata Kagere akifikia au kuivunja rekodi yake, bado mimi nitaendelea kuwa mfungaji bora wa kihistoria kwa upande wa wachezaji wazawa, halafu mashabiki lazima wajue, nilikuwa nafunga kwenye mazingira magumu na timu tunazokutana nazo ni ngumu kwelikweli,” alisema.

Kagere aliwahi kukaririwa, anafurahia kufunga na sio kwa lengo la kuvunja rekodi ya mtu, furaha yake kuona Simba inafaidika kwa gharama ilizotoa kumsajili Msimbazi na kwa sasa katika mechi 10 ilizonazo timu yake, anatakiwa kufunga mabao nane tu aandike rekodi mpya Tanzania.