KIMENUKA: Liverpool kuzuiwa kucheza Anfield

Monday June 29 2020
liver pic

Merseyside, England. ACHANA kabisa na kitu kinaitwa ukame, unaweza kufanya mambo ambayo hayakubaliki. Ndivyo ilivyo huko jijini Merseyside ambapo, mashabiki na wapenzi wa Liverpool wamelianzisha kila mtaa kushangilia ubingwa.

Tangu usiku wa Alhamisi baada ya Chelsea kuwachapa Manchester City kwa mabao 2-1 na kuwapa nafasi Liverpool kutangazwa mabingwa, mashabiki wa mabingwa hao wapya wa Ligi Kuu England, hawalali wala kufanya kazi ni kushangilia mitaani tu.

Liverpool ndio klabu ya Ligi Kuu England yenye mashabiki wenye mzuka mkubwa wanaposhangilia timu yao huku kuanzisha vurugu iwe nyumbani ama ugenini ni dakika sifuri, na jambo hilo limeanza kuwapa hofu watawala na kutangaza hali ya hatari.

Makundi makubwa ya mashabiki yamekuwa yakizunguka kwenye mitaa mbalimbali na kusababisha uchafuzi wa mazingira na sasa mamlaka imeonya kwamba, itaanza kuchukua hatua mbadala kuwadhibiti.

Taarifa zinaeleza kuwa, Mamlaka za Serikali zimeonya kuwa kama hali hiyo itaendelea basi Liverpool itapigwa marufuku kutumia Uwanja wa Anfield kwenye mechi zake za Ligi Kuu England zilizobaki.

Hatua hiyo ambayo imeungwa mkono na Polisi na hata klabu inalenga kuhakikisha hali ya utulivu inarejea kama zamani kwani, mashabiki hao wamesahau kama kuna janga la corona na maelekezo ya wataalamu wa afya ni lazima wafuatwe.

Advertisement

Polisi wa Merseyside na Meya wa Jiji hilo, Joe Anderson, kwa nyakati tofauti wamekemea vitendo vinavyoendelea kwa mashabiki hao kwamba, vinakiuka tahadhari za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Taarifa ya pamoja ya Polisi, klabu na Ofisi ya Meya, imesema kuwa vitendo vya makundi ya mashabiki hao kukusanyika eneo la Pier Head katikati ya jiji hilo, kushangilia ubingwa huo havikubaliki kwa wakati huu.

Taarifa hiyo imeeleza kwamba, kuna hofu kuwa mashabiki hao wanaweza kusambaa nje ya Anfield wakati chama lao linapokuwa uwanjani kutokana na mzuka walionao kwa sasa.

Kwa maana hiyo, mamlaka hizo zinakusudia kufuta kwa muda leseni ya matumizi ya Anfield kwa sababu za kiusalama kama mashabiki hao hawatakoma kushangilia kwa kuandamana mitaani.

Liverpool bado wana mechi saba mkononi na kati ya hizo tatu itakipiga kwenye dimba la nyumbani, Anfield ikiwemo ile ya Aston Villa, Burnley na Chelsea ambao waliwapa taji kwa kuwachapa Man City.

Ni hapo kwenye mechi dhidi ya Chelsea ndipo mamlaka zimeanza kuumiza kichwa kwani, ndio imepangwa kwa Liverpool kukabidhiwa rasmi taji hilo la ubingwa.

Taarifa za ndani zinasema kwamba, katika kuhakikisha amani na hofu ya kusambaa zaidi kwa virusi vya corona inadhibitiwa, mkakati uliopo ni kuangalia kama Liverpool wanaweza kukabidhiwa taji uwanja mwingine tofauti na Anfield.

Mkuu wa Polisi wa Merseyside, Andy Cooke amesema watu 15 wametiwa mbaroni kwa kuhusika kwenye matukio ya uhalifu wakati wa maandamano hayo ya mashabiki mitaani.

“Kinachofanyika kwa sasa ni kuharibu taswira ya mji wetu na klabu kwa ujumla…tuna wajibu wa kuendelea kudhibiti maambukizi ya corona lakini, wanachokifanya hawa hakikubaliki,” alisema Cooke.

Advertisement