Julio awapiga 'stop' makocha wazawa kuinoa Simba

Muktasari:

Julio hana timu anayoifundisha kwasasa baada ya kutimliwa kwenye klabu ya Dodoma FC kutokana na kushindwa kufikia malengo.

ALIYEKUWA kocha wa Dodoma FC, Jamhuri Kihwelo 'Julio', amesema kwa uwekezaji uliopo Simba hakuna kocha mzawa ambaye anaweza kuaminika kuwa kocha mkuu ingawa ameshauri viongozi kuanza kuwaamini makocha wazawa.

Julio ambaye kwasasa hana majukumu kwenye timu yoyote akiwa kama kocha amefunguka hayo siku chache baada ya kuhusishwa kutimuliwa kwa Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Ausems raia wa Ubelgiji na kuweka wazi kuwa kocha yoyote mzawa asijaribu kuomba kazi klabuni hapo.

Alisema kocha aliyeachiwa mikoba na Ausems hana muda mrefu kikosini hapo naye ataondolewa ni kutokana na uwekezaji uliopo klabuni hapo kuhitaji kocha mwenye mipango na misimamo kwa wachezaji wasumbufu.

"Simba wanahitaji matokeo mazuiri muda wote hawataki ubabaishaji ni kutokana na uwekezaji uliopo kuwa tayari kusajili mchezaji yeyote anayehitajika na pia wazawa tumekuwa hatupewi vipaumbele hasa kwenye kuzinoa Simba na Yanga ambazo zinaendeshwa na presha ya mashabiki," alisema.

"Sipo tayari kupeleka maombi yangu klabuni hapo kwani hata nikipata siwezi kuwa na muda mrefu klabuni hapo kutokana na presha ya mashabiki ikiwa ni sambamba na timu kuhitaji matokeo zaidi na wanachoangalia ni kocha wala sio wachezaji, ukocha ni kazi ya kuajiriwa na kutimuliwa nalitambua hilo lakini sio kwa hali  iliyopo Simba kwa sasa," alisema.

Kwasasa Simba, ipo chini ya kocha msaidizi Denis Kitambi ambapo inadaiwa mchakato wa kusaka kocha mpya umeanza huku Aussems huenda wakamalizana naye kesho Alhamis ambapo wana kikao cha pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Simba, Senzo Mazingisa.